Wadau Wapongezwa Kwa Kuchangia Miradi Ya Maendeleo
Serikali Mkoani Geita imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ambao wanajitoa kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Cornel Magembe alipokuwa akiongea na hadhara ya watu waliojitokeza kushuhudia makabidhiano ya vyumba saba vya madarasa na ofisi mbili za walimu katika Shule ya Msingi Nyamalembo ambavyo vimefanyiwa ukarabati na kampuni ya Usafirishaji Blue Coast Investment yenye makao makuu mjini Geita.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Cornel Magembe ametoa pongezi za dhati kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Blue Coast Ndugu Ignas Athanas kwa namna kampuni yake ilivyojitoa katika kuhakikisha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji katika Shule ya msingi Nyamalembo yanaboreshwa na kuwaalika wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano kutoka katika kampuni hiyo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya madarasa hayo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Blue Coast ambaye pia ni mlezi wa Shule ya msingi Nyamalembo ameeleza kuwa baada ya kukabidhi chumba kimoja cha darasa chenye samani zote ndani yake mwishoni mwa mwezi Juni 2023 wananchi wa Kata ya Mtakuja wakiongozwa na Diwani wao Mhe. Costantine Morandi Mtani walimuomba awasaidie kukarabati madarasa chakavu shuleni hapo, suala ambalo alilipokea kwa mikono miwili na kufanikiwa kulitekeleza ndani ya kipindi kifupi.
Diwani wa Kata ya Mtakuja ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Mhe. Costantine Morandi ametoa shukrani kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Blue Coast kwa kazi kubwa aliyoifanya katika Shule ya msingi Nyamalembo, ni Fahari kubwa kwao na pia ni ishara ya mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Kampuni hiyo na jamii inayowazunguka. Mhe. Morandi ameahidi kwa niaba ya wananchi wake kuwa watayatunza kikamilifu madarasa hayo ili yaendelee kuvutia na kuwanufaisha wanafunzi.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Nyamalembo Ndugu Josiah Mwombeki ameeleza kuwa ukarabati wa madarasa saba uliofanywa na Kampuni ya Blue Coast umewezesha kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ambapo wanafunzi watajifunza wakiwa katika mazingira safi na salama, kupunguza utoro kwa wanafunzi kwani kutawafanya wapende kuhudhuria shuleni na kumaliza uhaba wa madarasa 12 uliokuwepo ambapo kwa sasa madarasa na samani ni toshelevu kwa wanafunzi wote.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa