Wachimbaji Wadogo Waagizwa Kutumia Fursa za Vituo Vya Mafunzo
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Ndugu Msafiri Mbibo amewashauri wachimbaji wadogo mkoani Geita kutumia vituo vya mfano vya uchimbaji na uchenjuaji dhahabu vilivyopo mkoani hapo ili viwasaidie kujifunza namna bora ya kuchimba kwa teknolojia ya kisasa pasipo kuathiri mazingira.
Ndugu Mbibo ameyasema hayo hivi karibuni alipotembelea maonesho ya tano ya teknolojia ya madini yanayoendelea katika viwanja vya eneo maalum la uwekezaji kiuchumi Bombambili mjini Geita akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo.
Serikali ilianzisha vituo vya mfano vya Katente na Lwamgasa ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata ujuzi wa uchimbaji bora na wa kisasa hivyo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya madini anatarajia wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa kufuata taratibu zote ikiwemo utafiti na namna ya kuchimba kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kupata masoko ya bidhaa za madini.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo mkoani Geita Bwana Christopher Kadeo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwawezesha mbinu mbadala za kuchimba kisasa na kwamba kwa sasa wameanza kuachana na matumizi ya magogo na kwenda kwenye teknolojia ya kutumia vyuma kunyanyua mizigo kirahisi.
Kwa upande wake msimamizi wa kituo cha mfano cha kuchimba na kuchenjua dhahabu cha Lwamgasa, Victor Augustine amesema uwepo wa kituo hicho umewasaidia wachimbaji wadogo kuchimba kwa usalama na njia bora zaidi tofauti na miaka ya nyuma.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa