Waathirika wa Mvua Wametakiwa Kutunza Misaada
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Cornel Magembe amewaasa wananchi wa Kata za Kasamwa, Kanyala, Shiloleli na Bulela ambao nyumba zao ziliathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha zikiambatana na upepo kuanzia Oktoba 18 hadi Novemba 10, 2023 kuhakikisha misaada waliyopatiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wahisani wengine watakaojitolea inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mhe Magembe ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akigawa msaada kwa waathirika hao kutoka Tarafa ya Kasamwa, shughuli ambayo ilifanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Kata ya Kasamwa ambapo amewataka waathirika wa mvua hizo kutumia vyema misaada hiyo na kuwaelekeza watendaji kufuatilia ili kuhakikisha misaada iliyotolewa haiuzwi wala kutumika kinyume na malengo.
Akiwasilisha taarifa ya maafa mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mratibu wa maafa Halmashauri ya Mji Geita Bi. Valeria Makonda amesema kuwa takribani nyumba 556 za makazi ya watu katika tarafa ya Kasamwa zimepata madhara yakiwemo kubomoka kabisa, kuezuliwa mapaa na kupata mipasuko.
Bi. Makonda ameeleza kuwa Halmashauri ya Mji imepokea vifaa vya msaada wa kibinadamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya maafa. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mahindi tani 22.1, magodoro 71, mablanketi 148, mikeka 148, ndoo 74 madumu 74 na vyombo seti 40.
Mratibu wa Maafa Geita Mji ameongeza kuwa tofauti na makazi ya watu mvua hizo zimeathiri Taasisi mbalimbali ambazo ni madarasa 28 ya shule za Msingi na Sekondari, nyumba mbili za walimu, Zahanati moja, Kituo kimoja cha afya, Ofisi moja ya Serikali ya mtaa, makanisa 9 na msikiti 1 ambapo kutokana na tathimini iliyofanyika katika majengo na taasisi za umma jumla ya shilingi 225,461,080 zinahitajika ili kukarabati na kujenga miundombinu iliyoathirika.
Kamati za maafa za Kata kwa kushirikiana na Kamati ya maafa ya Halmashauri wameendelea kutoa elimu juu ya kuhama katika maeneo ya mabonde ambayo ni hatarishi katika kipindi cha mvua. Pia wananchi wameendelea kushauriwa kutotumia au kubomoa kabisa majengo ambayo ni hatarishi ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza. Aidha wameendelea kushauriwa kutekeleza kampeni ya ujenzi wa nyumba bora kwa kutumia tofali za kuchoma au tofali mfungamano ambazo ni gharama nafuu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa