Wananchi watakiwa Kuthamini zoezi la uandikishaji Uraia
Wananchi wanaoishi katika maeneo yote ya Halmashauri ya Mji Geita wametakiwa kutumia fursa iliyotolewa na Serikali ya awamu ya tano kupitia mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kujiandikisha kwa lengo la kupata vitambulisho vya uraia na kutambulika.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Geita Ndg. Herman C. Kapufi wakati wa uzinduzi rasmi wa zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wakazi wote katika Halmashauri ya Mji Geita. Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Ofisi ya Kata ya Kalangalala.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ameongeza kuwa wananchi wajitokeze kwa wingi katika zoezi hili kwani vitambulisho vya Taifa vitahakikisha raia wote wa Tanzania wanapata huduma stahiki za msingi na kijamii kama kupata malipo ya pensheni, haki za matibabu, haki za kujiunga na masomo, kujiunga na mifuko ya jamii na kumiliki ardhi. Pia itasaidia suala la usalama katika nchi kwa kuzingatia muingiliano wa watu uliopo nchini na matendo ya kigaidi yanayoendelea Duniani.
Ndg. Herman Kapufi ametoa rai kwa Maafisa watendaji na wenyeviti wa mitaa kushirikiana na mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kufanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa, hususani katika kuepuka uhujumu wa aina yoyote katika wilaya ya Geita kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Mhandisi Modest Apolinary amesema kuwa Halmashauri itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa( NIDA) katika kulinda usalama wakati na baada ya zoezi, kuelimisha umma, kuhamasisha na kuhakikisha wananchi wote wenye sifa na vigezo wamesajiliwa na kupatiwa kitambulisho cha Taifa. Pia kuweka na kuanzisha matumizi bora ya kitambulisho.
Tangu kuanza kwa zoezi la usajili na utambuzi wa watu wanaoishi katika Halmashauri ya Mji wa Geita mwezi Agosti 2017 zaidi ya watu 1,034,000( laki moja na elfu thelathini na nne) sawa na asilimia 75.33% wameshaandikishwa. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa imeahidi kuanza kugawa vitambulisho vya wananchi hao kuanzia mwezi Januari 2018. Kauli Mbiu ikiwa ni “ Kitambulisho cha Taifa kwa Usalama na Maendeleo ya Taifa.”
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa