Viongozi Watakiwa Kutunza Usafi wa Mazingira
Viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Vitongoji wameagizwa kuonyesha jitihada za dhati katika kujituma kwa kushirikiana na wananchi wanaowaongoza kutunza usafi wa mazingira katika maeneo yanayowazunguka.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel aliposhiriki katika zoezi la usafi wa mazingira katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Geita na maeneo mbalimbali ya mitaa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita pamoja na vijana wanaoshiriki mafunzo ya jeshi la akiba katika Wilaya ya Geita tarehe 25/07/2018, ikiwa ni siku ya kuwaenzi mashujaa wa Taifa la Tanzania waliotangulia mbele ya haki.
Kwa upande wake Mshauri wa jeshi la akiba katika Mkoa wa Geita, Luteni Kanali Daniel Mwadekela Mhagama amesema kuwa ni desturi ya majeshi ya ulinzi tarehe 25 Julai kila mwaka kuwaenzi mashujaa ambao wametangulia mbele ya haki katika harakati za kuikomboa nchi ya Tanzania wakiwemo wale walioshiriki vita vya Kagera ambao wamezikwa eneo la Kaboya mkoani Kagera. Pia mashujaa waliopambana kupinga ukoloni akiwemo Chifu Mkwawa, Mirambo na wengineo.
“ Tumeamua kuwaenzi mashujaa wetu kwa kufanya usafi katika mitaa mbalimbali ya Halmashauri ya Mji wa Geita ili kuungana na wenzetu ambao wako jirani na makaburi ya kaboya na nalilendele, Mtwara ambao siku ya leo wanafanya usafi katika makaburi hayo .” Aliongeza Luteni Kanali Mhagama.
Mshauri wa Jeshi la akiba katika Mkoa wa Geita amesema kuwa licha ya majukumu mengi yanayotekelezwa na Jeshi la Wananchi, jeshi hilo linafanya kazi ya kufufua uzalendo hususan kwa kuwafundisha vijana wa jeshi la akiba ili watambue kwamba kazi ya kulinda Mkoa wa Geita na nchi nzima kwa ujumla ni shughuli ya kujitolea.
Mkuu wa Idara ya usafishaji na mazingira katika Halmashauri ya Mji wa Geita Ndg. Fredrick Linga amesema kuwa hali ya usafi katika mji wa Geita sio ya kuridhisha sana kwa sababu wananchi bado wanatupa taka hovyo barabarani. Hivyo ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kutiririsha maji machafu barabarani na kushiriki katika shughuli ya usafi wa mazingira kila jumamosi ya mwisho wa mwezi katika nyumba zao, mazingira yao ya kazi na mji mzima kwa ujumla.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa