Vijana, Wanawake, Watu wenye ulemavu Geita Mji Wapatiwa Milioni 233
Halmashauri ya Mji wa Geita kupitia mapato yake ya ndani imefanikiwa kutoamikopo ya shilingi milioni 233 kwa vikundi 49 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ambapo vijana wamepewa mkopo wa shilingi 107,000,000/-, vikundi vya wanawake shilingi 123,000,000 na watu wenye ulemavu wamepewa mkopo wa shilingi 3,000,000/=
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi kwa vikundi hivyo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Geita Tarehe 13/10/2020, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhandisi Modest Apolinary amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 wametenga jumla ya shilingi 735,987,571 kwa ajili ya mikopo kwa makundi maalum ikiwa ni asilimia 10 ya mapato yake ya ndani.
Mhandisi Modest Apolinary ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2020 halmashauri yake imeshatoa shilingi Bilioni 2.5 kama mikopo kwa vikundi vya ujasiriamali vinavyoendeshwa na vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Akikabidhi mfano wa hundi kwa wawakilishi wa wanufaika wa mikopo hiyo Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amewataka waitumie vyema mikopo waliyopata katika shughuli za uzalishaji mali ili kujiletea maendeleo kwa kuhakikisha mnajituma kufanya kazi na kuondoa dhana ya kufikiri fedha hizo ni hisani au sadaka bali kwa mujibu wa sheria mnapaswa kuzirejesha kikamilifu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Costantine Kanyasu amesema kuwa utoaji wa mikopo hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwka 2015-20120 na kumshukuru Mkurugenzi wa Mji wa Geita kwa kuendelea kutekeleza mpango huo wa kutoa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu hata baada ya Baraza la Madiwani kuvunjwa.
Akiwasilisha taarifa ya utoaji mikopo Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Ndg. Majagi Maiga amesema kuwa katika kuhakikisha mfuko huo utatekeleza majukumu yake kwa ufanisi idara imeendelea kutoa elimu kwa wajasiriamali kuendelea kurejesha fedha hizo kwa wakati ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine zaidi kuweza kukopeshwa.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa