Halmashauri ya Mji Geita yazindua kampeni ya Ujenzi wa vyumba vya madarasa na zahanati
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameshiriki uchimbaji msingi wa nyumba ya walimu katika shule ya Msingi Shinamwendwa, ujenzi wa Shule ya Sekondari Mgusu na ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Nyakato katika Halmashauri ya Mji Geita.
Akizindua miradi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita amepongeza jitihada inazofanywa na wananchi kwa kutambua raslimali za asili zinazopatikana katika maeneo yao na kuzitumia. Pia kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo licha ya kuwepo changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao.
Amesema kuwa viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya vitongoji hadi wilaya wawatie moyo wananchi hao na kutunza heshima ya dhamana ya uongozi waliyopewa katika jamii kwa kushirikiana na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya ujenzi iliyoanzishwa ambayo imeibuliwa na wanachi wa maeneo mbalimbali katika Halmashauri ya Mji wa Geita.
“ Wananchi wana kiu ya maendeleo na watu mtakaotimiza malengo yao ni viongozi hivyo mjitahidi kuwa waadilifu na wachapakazi ili kuwaridhisha wananchi na Serikali yao, kama namna Serikali ya awamu ya tano inavyounga mkono jitihada za wananchi wake”.Aliongeza Mkuu wa Mkoa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Geita Ndg. Herman Kapufi amesema kuwa kuna baadhi ya wananchi ambao bado wana mtazamo wa kujengewa majengo yote na kutimiziwa mahitaji muhimu na Serikali pekee pasipo kuchangia chochote, hivyo mwananchi yeyote atakayekaidi kuchangia au kujitolea nguvu kazi katika shughuli za ujenzi aripotiwe katika ofisi yake na kuchukuliwa hatua madhubuti.
Mkuu wa Mkoa wa Geita alikuwa katika ziara ya kikazi yenye lengo la kuibua miradi ya majengo ya shule na zahanati ili kutimiza malengo ya kuwa na zahanati kwa kila kijiji kufikia mwaka 2020 na kujitahidi kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa katika Mkoa wa Geita ambapo mahitaji ni vyumba 8600 na vilivyopo sasa ni vyumba 571.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa