Ujenzi wa Vibanda Soko kuu Geita Awamu ya Pili wazinduliwa
Halmashauri ya Mji wa Geita imezindua rasmi ujenzi wa vibanda vya maduka yanayozunguka soko kuu mijini Geita ambapo awamu ya kwanza ya ujenzi wa vibanda vya maduka unaendelea na unataraji kukamilika mwezi Juni 2019.
Akizindua rasmi ujenzi huo tarehe 27/2/2019 katika eneo la soko kuu Geita Mjini, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amepongeza Halmashauri ya Mji wa Geita na Mgodi wa Dhahabu wa Geita(GGM) ambao ndio wafadhili wa mradi kwa kuibua na kuwezesha ujenzi wa mradi huo kufanikiwa.
Mhandisi Robert Gabriel amewaagiza viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita kusimamia mradi huo kikamilifu bila kuchakachuliwa, pia amemtaka mkandarasi M/S Magacon anayejenga mradi huo kumaliza ujenzi huo kwa muda uliopangwa ili wananchi warejee kufanya biashara zao na kuinua uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Mji Geita, Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Leonard Bugomola ameahidi kuusimamia mradi huo kikamilifu na kusema kuwa vitakuwa ni vibanda vyenye hadhi ya kimataifa. Pia ametumia fursa hiyo kuwaahidi wafanyabiashara wote ambao vibanda vyao vilivunjwa kupisha ujenzi wa mradi huo kuwa watapewa kipaumbele cha kupata vibanda kabla ya wafanyabiashara wapya kupatiwa eneo.
Mhe. Bugomola amesema kuwa mradi huo utaongeza mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kupangisha vibanda kwa wafanyabiashara, uwezo wa Halmashauri kuhudumia wananchi wake katika kata mbalimbali utaongezeka kwa sababu ya wingi wa mapato yatakayopatikana kutoka katika chanzo hicho. Kadhalika mradi utabadilisha na kuboresha mandhari na muonekano wa eneo na kuwa moja ya kivutio katika mji wa Geita.
Mradi wa ujenzi wa vibanda vya biashara katika soko kuu la Geita ulibuniwa na Halmashauri ya Mji kama mradi wa kimkakati ili kukuza uchumi wa Halmashauri kwa kuongeza mapato ya ndani, ambapo ujenzi huo kwa awamu ya kwanza na pili umetengewa kiasi cha fedha za kitanzania 2,300,000,000/= kutoka katika fedha za huduma kwa jamii( CSR) zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita( GGM) . Ujenzi wa vibanda kwa awamu ya pili unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2019.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa