Ujenzi wa Miundombinu Ya BOOST Waanza Kwa Kishindo
Ujenzi wa vyumba vya madarasa, mashimo ya vyoo na shule mpya za msingi umeanza kutekelezwa Kupitia mradi wa BOOST katika Halmashauri ya Mji Geita.
Mwamko huo umekuja baada ya agizo la Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Cornel Magembe hivi karibuni alipokuwa akizungumza wakati wa kikao cha baraza la Madiwani kilichoketi katika ukumbi wa EPZ Bombambili Geita mjini.
Mhe. Magembe ametoa shukrani za dhati kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha wilaya ya Geita fedha ambazo zinaendelea kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Wasimamizi wote wa mradi katika wilaya ya Geita hakikisheni utekelezaji wa mradi wa BOOST unaanza haraka, kadhalika miradi yote inayoendelea kujengwa ikamilishwe kwa wakati ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi ndani ya muda uliopangwa.” Aliongeza Mkuu wa Wilaya ya Geita.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhe. Costantine Morandi ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutambua uwepo wa halmashauri yake kwa kuwapatia fedha nyingi zinazotumika katika ujenzi wa miundombinu katika Shule za msingi. Pia ameahidi kusimamia kikamilifu miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi
Kupitia mradi wa BOOST Halmashauri ya Mji Geita imepokea Shilingi 1,653,300,000/= ambazo zitatumika kujenga vyumba 18 vya madarasa katika shule mbalimbali, madarasa mawili ya mfano kwa elimu ya awali, chumba kimoja cha darasa la elimu maalum na matundu 13 ya vyoo.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa maagizo kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha zinazotolewa katika utekelezaji wa miradi hiyo zinakamilisha ujenzi kama ilivyopangwa ili kuepusha miradi mingi kutokamilika huku fedha zikiwa zimekwisha. Pia thamani ya fedha itakayotolewa iendane na majengo yatakayojengwa ili kufikia matokeo yaliyokubalika.
Mradi wa BOOST utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021/2022 hadi 2025/2026 ambapo utatekelezwa kwa awamu tofauti. Mkoa wa Geita umepokea Shilingi 9,781,100,000 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 11, vyumba vya madarasa 143 ya Shule za Msingi, vyumba vya madarasa ya mfano ya Elimu ya Awali 12, chumba kimoja cha darasa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum na matundu 94 ya vyoo.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa