Ujenzi wa Madarasa 71 Waanza Kwa Kasi Geita Mji
Ujenzi wa vyumba 71 vya madarasa katika Shule 12 za sekondari zilizoko katika Halmashauri ya Mji wa Geita umeanza kutekelezwa ambapo wananchi wa maeneo husika kwa kushirikiana na mafundi wazawa wamejenga msingi wa majengo hayo na kwa sasa iko katika hatua za ukamilishwaji.
Akizungumza na mwandishi wa Habari hii hivi karibuni Mkuu wa idara ya ujenzi Halmashauri ya Mji wa Geita Mhandisi Makongoro Igungu amesema kuwa ujenzi wa misingi ya madarasa katika shule zote 12 ambazo zinatekeleza mradi huo umeshaanza ambapo umewashirikisha wananchi wa maeneo husika na kwa sehemu kubwa ujenzi wa hatua ya msingi uko katika hatua za ukamilishaji.
Mhandisi Igungu ameeleza kuwa idara yake kwa kushirikiana na idara ya elimu Sekondari imejipanga kikamilifu katika usimamizi na ufuatiliaji wa ujenzi huo na kwamba watahakikisha ujenzi unakamilika ndani ya muda uliopangwa na kujenga madarasa yenye viwango vya hali ya juu kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza 2023 kupata mahala pa kujifunzia.
Hivi Karibuni Halmashauri ya Mji wa Geita ilipokea jumla ya Shilingi 1,420,000,000( Bilioni 1.4) kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 71 vya madarasa ambayo yatatumiwa na wanafunzi wanaotaraji kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023 katika shule 12 zilizobainika kuwa na uhitaji Zaidi wa madarasa ya msingi.
Shule zilizopokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2023 ni pamoja na Shule ya Sekondari Bombambili, Bulela, Ihanamilo, Kalangalala, Kisesa, Kivukoni, Lukaranga, Mkangala, Mwatulole, Nyabubele, Nyanguku na Shantamine ambapo kila chumba cha darasa kitajengwa kwa shilingi milioni 20.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa