Tunzeni Vitabu Viwatunze – RC Shigela
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela amewaasa walimu na wanafunzi wilayani Geita kuhakikisha wanavitunza na kutumia kwa malengo vitabu vya sayansi ili viweze kuwasaidia watoto ambao watapata ujuzi utakaozalisha wanasayansi watakaoliwezesha Taifa kupiga hatua Zaidi katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia.
Mhe. Shigela ametoa kauli hiyo hivi karibuni alipokuwa akipokea jumla ya vitabu 52,683 vya masomo ya Hisabati, sayansi, Kiswahili na kingereza kwa shule 87 za msingi kuanzia darasa la nne hadi saba na vitabu vya kusoma, kuandika na kuhesabu kwa darasa la kwanza na pili, vifaa vya michezo na kujifunzia kwa watoto wenye ulemavu ambavyo vimetolewa na Shirika la Plan International, ambapo vitabu 43,800 kati ya hivyo vimenunuliwa kupitia mradi wa kuwawezesha wasichana kuendelea na masomo kwa kifupi KAGIS( Keeping Adolescent Girls in School) kwa ufadhili wa nchi ya Canada
Mkuu wa Mkoa wa Geita amelishukuru Shirika la Plan International kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuwathamini wanafunzi na watoto wa Geita kama ambavyo imezoeleka jamii kubwa ya kanda ya ziwa haitoi kipaumbele cha kumpatia elimu mtoto wa kike.
“Nawaagiza walimu wote ambao mmekabidhiwa vitabu muhakikishe mnatengeneza maktaba nzuri na zenye ubora ambazo mtazitumia kutunza vitabu hivyo ambavyo vitatumika kufundishia na wanafunzi watawekewa utaratibu maalum utakaowawezesha kusoma pasipo kufanya uharibifu kama kuchana kurasa za ndani na uharibifu mwingine”. Aliongeza RC Shigela.
Akishukuru kwa niaba ya uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Egidy Teulas amesema kuwa ni vigumu kutaja maendeleo ya wilaya ya Geita pasipo kuwataja Plan Internationl kutokana na mchango mkubwa ambao wanatoa kwa jamii hususan katika masuala ya haki za watoto. Pia ameahidi kushirikiana na walimu wake kuvitunza vitabu walivyopewa ili view na manufaa kwa watoto ambao ni Taifa la kesho.
Kwa upande wake Meneja wa mradi wa KAGIS Ndg. Nicodemus Gachu ameeleza kuwa shirika la Plan International linatambua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu kama upungufu wa vitabu, nyumba za walimu hivyo wakaona ni vizuri wakaisaidia Serikali katika kupunguza mzigo mkubwa wa mahitaji kwa kutoa vitabu hivyo ambavyo vimenunuliwa kwa Zaidi ya shilingi milioni 438 za kitanzania.
Ndg. Gachu ameeleza kuwa kupitia mradi wa KAGIS jumla ya vyoo 50 vitajengwa katika shule za mradi kwenye mikoa ya Geita na Kigoma. Kadhalika kwa kipindi cha miaka mitano mradi utanunua na kusambaza jumla ya baiskeli 2200 kwa watoto wa kike wanaolazimika kutembea umbali mrefu kwenda shuleni pamoja na kutoa mafunzo juu ya afya ya uzazi na usawa wa kijinsia.
Mradi wa KAGIS ambao unatekelezwa katika mikoa ya Geita na Kigoma kwa miaka mitano umelenga kushughulikia changamoto zinazozuia wasichana walio katika umri balehe kutambua haki yao ya elimu salama, bora na inayozingatia jinsia pamoja na hayo mradi unachangia kutimiza malengo ya wizara ya elimu, sayansi na teknolojia katika kuhakikisha upatikanaji sawa na kukamilika kwa elimu ya msingi kwa wote.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa