TUMIENI HEKIMA KUTUNZA MAZINGIRA- DC
Wakazi wa Wilaya ya Geita wametakiwa kutumia busara na hekima katika utunzaji wa mazingira katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii wanazozifanya.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Ndg. Herman Kapufi wakati akihutubia hadhara iliyoshiriki maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika kiwilaya katika kata ya Mgusu, Halmashauri ya Mji wa Geita tarehe 5/06/2018.
Ndg. Herman Kapufi amewasihi wananchi kuwa na nidhamu ya kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalam wa mazingira kwa kuacha tabia ya kukata miti hovyo, kutunza vyanzo vya maji, kutotupa taka hovyo na kutumia nishati mbadala ya gesi na mkaa unaotumia mapumba badala ya mkaa wa miti unaotumika kwa wingi hivi sasa.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ameongeza kuwa waharibifu wa Mazingira waonywe ili waache tabia ya kuharibu mazingira kiholela . Pia kila kaya ihakikishe inapanda miti ya aina mbalimbali kama ya matunda , kivuli na mbao ili kukabiliana na uchafuzi wa hali ya hewa.
Akizungumzia baadhi ya mikakati iliyowekwa na Wilaya ya Geita, Ndg. Kapufi amesema kuwa uongozi wa Wilaya ya Geita umedhamiria kufanya doria za mara kwa mara katika hifadhi za misitu, kutoa elimu kwa jamii iliyopakana na hifadhi, kugawa mbegu na miche ya miti ili kuweza kutunza mazingira, kuwafukuza wachimbaji wadogo wa dhahabu wanaochimba ndani ya hifadhi ya misitu.
Maafisa Mazingira na usafishaji wa Halmashauri za Wilaya ya Geita na Geita Mji wamebainisha changamoto zinazoukabili mji wa Geita kuwa ni wimbi kubwa la uharibifu wa mazingira kupitia uvunaji miti kwa ajili ya nishati, madini, kilimo, malisho ya mifugo na makazi, tatizo la utupaji taka ngumu ovyo ambapo asilimia kubwa ya taka ina mifuko ya plastiki. Pia mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanasababishwa na ukataji na uharibifu wa misitu.
Afisa Mazingira na Usafishaji wa Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Pancrace Shwekelela amesema katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, jumla ya miti2, 157,535 imepandwa katika maeneo mbalimbali wilayani Geita. Ameongeza kuwa Idara ya Mazingira na udhibiti wa taka ngumu imekuwa ikisimamia shughuli za usafi wa Mazingira kwenye maeneo ya Umma kama mashuleni,kwenye masoko na maeneo ya wachimbaji wa dhahabu.
Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa tarehe 5 Juni kila mwaka kwa lengo la kuhimiza jamii kutunza, kuhifadhi na kulinda mazingira na pia kuepuka athari zinazotokana na uharibifu wa Mazingira. Ujumbe wa siku hiyo kwa Mwaka huu ni “MKAA NI GHARAMA: TUMIA NISHATI MBADALA.”
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa