Tumieni Fursa Zilizoko Geita- TD Geita
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Bi. Zahara Michuzi amewakaribisha Mabalozi wa Tamasha la Kutoa huduma na kutangaza shughuli za Maendeleo (ZIFIUKUKI) kutumia fursa zilizoko katika Mji wa Geita na mkoa kwa ujumla kwa lengo la kukuza uchumi na kuimarisha uwekezaji wa ndani.
Bi. Zahara ameyasema hayo Tarehe 29/11/2023 alipokuwa akizungumza na mabalozi hao waliofanya ziara ya kutembelea Halmashauri ya Mji Geita kwa lengo la kufahamu miradi inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita amewaeleza mabalozi hao kuwa Halmashauri yake inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo kwa kutumia fedha za Huduma ya Kampuni kwa jamii (CSR) kutoka Mgodi wa Dhahabu Geita(GGM), hivyo kupitia mradi huu mabalozi hao wamehamasishwa kufungua maduka ya kuuza vifaa vya michezo, maduka ya vinywaji na maduka ya mahitaji mengine.
Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wenzake msanii Simon Mwapagata amesema kuwa wamepokea mwaliko wa fursa hizo na watazifanyia kazi, pia wameahidi kuunga mkono jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutangaza shughuli za Serikali hususan utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo katika Mji wa Geita.
“Tunaipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuwatengenezea watanzania wote mazingira salama ya kuishi, sisi kama wasanii tunamuahidi kushirikiana naye katika kuhakikisha wananchi wote wanaitambua miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali”. Aliongeza Simon Mwapagata.
Miradi iliyotembelewa na mabalozi hao ambao ni wasanii wa filamu ni pamoja na ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa michezo Geita mjini, Ujenzi wa shule maalum ya sekondari ya wasichana inayojengwa kwa shilingi Bilioni 3 kutoka Serikali kuu, Ujenzi wa Shule mpya ya msingi Juhudi, Upanuzi wa Kituo cha afya Nyankumbu na Ujenzi wa Soko kuu la Dhahabu Geita mjini.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa