Timu Ya Halmashauri Yapata Udhamini Kutoka GGM
Timu ya Mpira wa miguu Geita Gold Footbal Club inayomilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Geita imeingia makubaliano na Mgodi wa Dhahabu wa Geita ambapo mgodi wa GGM utaidhamini timu shilingi Milioni 800 za kitanzania katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa makubaliano iliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Ofisi za Halmashauri ya Mji Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Wilson Shimo ametoa rai kwa uongozi wa timu pamoja na Halmashauri ya Mji Geita kutumia ujuzi na weledi mkubwa katika kuiongoza timu hiyo na kuweka mikakati mikubwa ya namna ya kuiendeleza ili kutunza alama na nembo ya mkoa wa Geita kwa kizazi cha sasa na baadaye.
Mkurugenzi Mtendaji wa mgodi wa GGM Ndugu Terry Strong amesema kuwa wamefikia uamuzi wa kuendelea kuwa wadhamini wa timu ya GGFC kwa misimu miwili sasa ambapo mwaka uliopita kampuni yake ilitoa udhamini wa shilingi Milioni 500. Shilingi Milioni 800 zilizotolewa na Mgodi wa GGM zitaiwezesha timu kupata basi, chakula cha wachezaji, jezi pamoja na mahitaji muhimu ya timu.
Mbunge wa jimbo la Geita mjini Mhe. Costantine Kanyasu amesema kuwa wananchi wa Geita wanajivunia uwepo wa Mgodi wa GGM na anaamini kuwa udhamini uliotolewa utaendeleza kiwango cha timu na kuwa chachu ya kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja. Pia amewaomba viongozi wa GGM kutoa udhamini kwa timu ya mpira wa miguu ya wanawake (Geita Queens) ambayo imeendelea kuutangaza mkoa wa Geita.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Bi. Zahara Michuzi ametoa shukrani za dhati kwa Mgodi wa GGM kwa kuongeza udhamini wa timu ya GGFC, udhamini huo utaleta tija katika maendeleo ya timu na jamii kwa ujumla. Pia amekaribisha makampuni na Taasisi nyingine kuja kutoa udhamini kwa timu yetu ya Geita Gold FC.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa