TFS Marufuku Kuwapiga Wananchi- Kanyasu
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Costantine Kanyasu amewaagiza watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania( TFS) kutowapiga wananchi wanapokuwa katika doria za ufuatiliaji wa mazao ya misitu hususani mbao na mkaa.
Mhe. Kanyasu ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Mgusu wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika tarehe 31/12/2019 katika uwanja wa senta ya Mgusu.
“Ni kosa la jinai na ni marufuku kwa watumishi wa TFS kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga wananchi wanaokamatwa wakiwa wamehujumu maliasili za misitu. Ukamataji wa waharibifu wa maliasili uwe wa kistarabu na si kutumia nguvu, Afisa Maliasili yeyote atakayetumia nguvu pasipokuwa na busara dhidi ya raia atachukuliwa hatua kali za kinidhamu. Kadhalika wananchi hamtakiwi kuwafanyia vurugu watumishi wa TFS wanapokuwa kazini.”Aliongeza Mhe. Kanyasu.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii amewataka watumishi wa TFS kuboresha mahusiano ya utendaji kazi kati yao na Halmashauri za miji, Wilaya, Manispaa na jijini. Pia amewasihi wananchi hususani wachimbaji wadogo wanaotumia magogo ya miti katika shughuli zao kulipia kwa utaratibu kabla ya kuyavuna.
Mhe. Kanyasu alitumia fursa hiyo kuwaasa wananchi wa kata ya Mgusu kutokuwa wazito katika kuchangia katika shughuli za maendeleo kama ujenzi wa zahanati ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Geita na ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Kulingana na taarifa ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Halmashauri ya Mji wa Geita ina eneo la mpaka wa msitu wa hifadhi km. 1,662.52 ambapo hali ya misitu ya hifadhi nne zilizoko katika Wilaya ya Geita sio nzuri kutokana na shughuli za kibinadamu zinazoendelea kufanyika ndani ya hifadhi kama vile uchomaji mkaa, kilimo, makazi, ukataji miti kwa ajil ya nguzo(matimba)na mbao, malisho ya mifugo na uchomaji moto.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa