Teknolojia ya Tofali Fungamano kupunguza Uhaba wa Madarasa
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameziagiza Halmashauri zote katika Wilaya ya Geita kuhakikisha wanatumia matofali fungamano( Interblocking) katika ujenzi wa miundombinu ya madarasa kwenye Shule za Msingi na Sekondari ili waweze kujenga madarasa mengi na kwa gharama nafuu.
Mhandisi Robert Gabriel amebainisha hilo wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Mji wa Geita hivi karibuni ambapo kwa kushirikiana na wananchi wa meneo hayo alichimba misingi ya ujenzi wa madarasa katika Shule za Msingi Mgusu na Uwanja katika kata ya Nyankumbu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amewahamasisha wananchi kutumia teknolojia hiyo kwa sababu kwa gharama ya shilingi milioni 11 tu ujenzi wa darasa moja na la kisasa unakamilika tofauti na matofali ya saruji ambapo darasa moja hujengwa kwa zaidi ya shilingi milioni 20.
Mhandisi Robert Gabriel alitumia fursa ya ziara hiyo kutoa darasa kwa viongozi wa Kata za Mgusu na Nyankumbu kwa kuwakumbusha viongozi hao kuwa wabunifu,waaminifu, waadilifu, wenye hekima na buasara, wanyenyekevu na wasio na tamaa. Pia kiongozi anatakiwa atambue raslimali zinazomzunguka na kutambua namna zitakavyoinufaisha jamii nzima.
Diwani wa Kata ya Nyankumbu Mhe. Paschal Sukambi amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa kuwapatia fedha za awali ambazo wamenunua saruji na matofali na kufanya ujenzi wa shule shikizi ya Uwanja kuanza ambaopo itakapokamilika itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule za Nyankumbu na Ukombozi pamoja na kuwanusuru wanafunzi na ajali za barabarani wanapovuka kutoka nyumbani kwenda shule na wakati wa kurudi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhandisi Modest Apolinary amewasihi wananchi wa Nyankumbu kubadilisha mitazamo na kushiriana na Serikali katika kuchangia shughuli za maendeleo. “Igeni mfano wa Kata za Shiloleli na Bung’wangoko ambazo ziko pembezoni mwa mji wa Geita lakini wamejitoa kwa hali na mali katika ujenzi wa maboma ya madarasa na baada ya hapo Halmashauri ilitoa fedha za ukamilishaji.” Aliongeza Mhandisi Modest Apolinary.
Matofali fungamano( Interblocking) ni matofali ambayo yanatumika katika ujenzi wa majengo kwa kuyapanga yenyewe pasipo kujengea kwa kutumia mchanga na saruji kama matofali mengine, matofali hayo yanatengenezwa na kikundi cha Nyakatoma Hyrdoform brick making kilichopo Gieta mjini ambao wameajiriwa na Halmashauri ikiwa ni mkakati wa Halmashauri kuwatumia vijana katika shughuli zake za maendeleo.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa