TASAF Kuwapunguzia Mwendo Wananchi wa Mkolani
Jumla ya kaya 921 zinazoundwa na mitaa ya Buchundwankende na Ilungwe kata ya Nyankumbu Halmashauri ya Mji Geita zitanufaika na uwepo wa Zahanati mpya ya Mkolani ambayo inajengwa kwa Shilingi Milioni 197.2 Kupitia mradi wa Maendeleo ya Jamii Nchini (TASAF)
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi huo hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Cornel Magembe ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujali afya za wananchi wake kwa lengo la kuhakikisha kila Kata inakuwa na Kituo cha Afya na Zahanati kwa kila Kijiji.
Mhe. Magembe amesema kuwa wananchi wa mitaa itakayonufaika walipata adha kubwa ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu katika Kituo cha Afya Nyankumbu na Zahanati ya Ikulwa, hali ambayo inawapa usumbufu wanawake wanaokwenda kujifungua , jambo ambalo linakwenda kuwa historia kutokana na kukamilishwa kwa Zahanati ya Mkolani.
Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji Geita Bw. Amani Madenge ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa Zahanati hiyo unatekelezwa kwa muongozo wa Kupunguza Umaskini awamu ya nne ambapo TASAF inashirikiana na uongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Mkoa hati mtaa na kusimamiwa na jamii kupitia kamati za usimamizi wa miradi (CMC).
“Tunatoa shukrani kwa TASAF kwa kuiwezesha jamii ya Mkolani kusogezewa huduma ya matibabu karibu na maeneo yao. Pili jamii kupitia Kamati za usimamizi zimejengewa uwezo katika suala la usimamizi wa miradi na manunuzi, hii itaongeza wananchi kuutunza vyema na kuusimamia mradi usiharibiwe kwa makusudi”. Aliongeza Bw. Madenge.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa