Taasisi Za Fedha Zaagizwa Kuondoa Urasimu
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezitaka Taasisi za kifedha nchini yakiwemo Mabenki mbalimbali kuondoa urasimu katika huduma wanazotoa ili kuwezesha wafanyabiashara wa kati na wadogo kupata huduma bila vikwazo.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Uwezeshaji Bi. Dorothy Mwaluko alipokuwa akizindua rasmi programu ya kuendeleza biashara katika Mkoa wa Geita katika viwanja vya Soko kuu la Dhahabu hivi karibuni.
Bi. Mwaluko amesema kuwa Mabenki na Taasisi nyingine za kifedha yamekuwa yakihubiri kutoa huduma nzuri kwa wafanyabiashara lakini kiuhalisia huwawekea wafanyabiashara hao masharti magumu yanayokuwa kizingiti kwao katika kupata mikopo ya kuendesha shughuli zao.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji la Taifa Bengi Issa amesema kuwa Baraza hilo limesaini mkataba wa makubaliano na Mgodi wa Dhahabu wa Geita( GGM) wa kuwezesha wafanyabiashara kwa muda wa mwaka mmoja
Kwa upande wake Rais wa Mgodi wa GGM Ndg. Simon Shayo amesema mgodi huo umetenga jumla ya Shilingi Bilioni moja kwa ajili ya kufadhili program hiyo ili kuhakikisha wafanyabiashara wanajengewa uwezo ili waweze kushindana katika kufanya biashara pamoja na Mgodi huo na sekta nyingine.
Baadhi ya wafanyabiashara katika Mkoa wa Geita wameuomba Mgodi wa GGM kupunguza masharti ili hata wajasiriamali wa kawaida wapatiwe kazi ndogo za kufanya biashara katika mgodi huo
Lengo la Programu hiyo ni kukuza viwango vya wafanyabiashara katika Mkoa wa Geita na kuhakikisha Sekta zisizo rasmi zinashiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya Taifa .
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa