Taasisi Za Fedha Kopesheni Kwa Riba Nafuu- DC
Taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na masuala ya kifedha zikiwemo benki katika Wilaya ya Geita zimeagizwa kukopesha mikopo yenye riba nafuu vikundi vya wanawake wanaojishughulisha na ujasiriamali katika Nyanja tofauti.
Agizo hilo limetolewa na mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Geita Wakili Innocent Mabiki ambaye ni Afisa Tarafa wa Geita akizungumza kama mgeni rasmi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya wanawake yaliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Gedeco Halmashauri ya Mji Geita.
Ndg. Mabiki amesema kuwa mikopo yenye riba kubwa ambayo inatolewa na taasisi za kifedha zilizoko katika maeneo yao zinawavunja moyo wanawake wote ambao wamekusudia kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali lakini wamekosa mitaji ya kuanzishishia biashara zao. Kadhalika amewakumbusha wanawake waliopata mikopo kujenga desturi ya kurejesha kwa wakati mikopo hiyo ili na wenzao wapewe.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji Geita Ndg. Majagi Maiga ameeleza kuwa wanawake wengi katika mji wa Geita wamepata mwamko wa kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo biashara ndogo ndogo, ufugaji, kilimo cha mazao ya chakula na biashara, ushonaji nk. Dhana ya kujihusisha na uzalishaji mali imeendelea kuwafanya kuwa wabunifu wa miradi ya maendeleo.
Ndg. Maiga amesema kuwa Idara yake hupokea baadhi ya changamoto zinazowakabili wanawake na Halmashauri ya mji wa Geita inaendelea kukabiliana nazo kwa kuendelea kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake ili kutangaza bidhaa zao na kuzikuza katika viwango vya ubora kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama SIDO, Kuhamasisha wanawake kuunda vikundi vyenye miradi yenye mwelekeo wa viwanda vidogo na kushirikiana na wadau wa maendeleo na Taasisi za kifedha ili kuwezesha wanawake wengi zaidi kupata fursa za kuwezeshwa kiuchumi.
Siku ya wanawake duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka kwa lengo la kuenzi na kutambua mchango wa wanawake katika shughuli za malezi,kijamii na kiuchumi ambazo huwezesha kusukuma gurudumu la maendeleo. Ambapo maadhimisho ya mwaka 2021 yaliongozwa na kauli mbiu isemayo “Wanawake katika Uongozi: Chachu kufikia Dunia Yenye Usawa.”
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa