Wazee Wote Wapatiwe Vitambulisho vya Matibabu- DC
Halmashauri ya Mji na Wilaya Geita zimeagizwa kuwa kufikia mwezi Disemba 2017 wazee wote ambao hawajapata vitambulisho vya matibabu wapewe ili kuwajengea mazingira rafiki katika upatikanaji wa huduma za afya.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Ndg.Herman C. Kapufi wakati wa maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani iliyofanyika kiwilaya katika kata ya Mgusu, Halmashauri ya Mji Geita tarehe 01/10/2017.
Mkuu wa Wilaya amesema kuwa wazee wote katika Halmashauri mbili zinazounda mkoa wa Geita wanatakiwa watambuliwe na kupatiwa matibabu bila gharama yoyote kufuatia agizo lililotolewa kwa nchi nzima na Waziri wa Afya Jinsia na watoto . Pia amewataka waganga/ wauguzi katika zahanati na vituo vyote vya afya watoe huduma za matibabu kwa wazee bila manyanyaso kwa sababu wanahitaji kupewa kipaumbele katika huduma za matibabu.
“Mzee yeyote atakayenyanyaswa au kudharauliwa wakati wa kupatiwa matibabu atoe taarifa katika ofisi yangu ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa dhidi ya mganga au muuguzi huyo.” Aliongeza Ndg. Herman Kapufi.
Mkuu wa Wilaya ya Geita alitumia muda huo kuwashauri wazee watambue fursa zilizopo katika maeneo yao ili watoe mapendekezo ya miradi ya kiuchumi itakayotekelezwa katika maeneo yao na kuwanufaisha. Kadhalika, aliwataka wazee ho kutowafichia siri vijana wao ambao ni wahalifu hususani wanaowatishia kuwaua, bali watoe taarifa za vijana hao kwenye vombo vya dola juu ya vitendo viovu wanavyofanyiwa.
Pia aliagiza kuundwa kwa mabaraza ya wazee kuanzia ngazi ya kata hadi Wilaya ili kutoa nafasi kwa wazee wote Wilayani Geita kuwa na chombo kitakachojadili masuala na changamoto zinazowakabili ikiwemo masuala ya ulinzi na usalama pamoja na ukatili kama mauaji ya vikongwe yanayofanywa dhidi ya wazee katika jamii.
Akisoma risala iliyoandaliwa na wazee , Mwenyekiti wa Umoja wa wazee katika Wilaya ya Geita Ndg. Laurent S. Galani amesema kuwa wazee Wilayani Geita bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama kutopatiwa mikopo ya makundi maalum, wazee kukosa nafasi ya uwakilishi katika maamuzi kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa kama ilivyo kwa vijana na wanawake. Pia asilimia kubwa ya wazee bado hawajapatiwa kadi za bima ya bure ya matibabu.
Jumla ya wazee 19186 wameshapatiwa vitambulisho vya bure kwa ajili ya matibabu, na wazee 7720 bado wanasubiri vitambulisho hivyo ambapo shughuli ya kuvitengeneza inaendelea. Siku ya wazee Duniani huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuwaenzi wazee wote na kuthamini mchango wao katika maendeleo ya Taifa. Ujumbe wa siku hii kwa mwaka huu ni “Kuelekea uchumi wa viwanda tuthamini mchango uzoefu na ushiriki wa wazee”.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa