Nyanza Kujengewa Choo Bora na cha Kisasa
Kampuni ya Uchimbaji Madini Ardhini( African Underground Mining Services) ambayo inafanya kazi ndani ya Mgodi wa Dhahabu Geita imetoa ahadi ya kujenga choo bora na cha kisasa kwa ajili ya wanafunzi wa kike wanaosoma katika Shule ya Msingi Nyanza Halmashauri ya Mji wa Geita.
Ahadi hiyo imetolewa na Meneja Mradi wa Kampuni ya AUMS Ndg. Tom (Chris) Sawyer hivi karibuni wakati wa hafla fupi ya kukabidhi madarasa matano na ofisi moja ya walimu ambayo yamefanyiwa ukarabati na kampuni yake, hafla iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nyanza.
Ndg. Sawyer amesema kuwa kampuni yake imeshirikiana na Serikali katika ukarabati wa Shule ya Msingi Nyanza ikiwa ni sehemu ya wajibu wa Kampuni kwa jamii inayowazunguka. AUMS inafurahi kuona vijana ambao ni nguvukazi ya Taifa wanapata elimu kwenye mazingira rafiki ndio maana watahakikisha wanafunzi wa kike ambao wanahitaji kupata choo wanajengewa mapema iwezekanavyo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameishukuru kampuni ya AUMS kwa kutambua thamani ya watoto na kutimiza wajibu wao, na ameiomba kampuni hiyo kuichukulia shule ya Msingi Nyanza kama sehemu yao na kuwaomba waisaidie Serikali kukarabati majengo ya madarasa yaliyosalia ambayo hayana muonekano mzuri.
“WanaGeita tuna mila yetu ya kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa na maendeleo ya kuigwa hivyo Mkuu wa Wilaya nakuagiza kuyaeleza makampuni mengine yanayofanya kazi ndani ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita kushirikiana na Serikali kwa kuchangia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kama ilivyofanya kampuni ya AUMS.” Aliongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Kijana Ally Salum ambaye ni mwanafunzi wa Darasa la saba katika Shule ya Msingi Nyanza ameishukuru Kampuni ya AUMS kwa kuwathamini na kuwafanya wasome kwenye madarasa ambayo yanalingana na shule za binafsi. Kadhalika kumalizika kwa ukarabati wa madarasa hayo kumewarahisishia walimu wao kufundisha kwa nafasi kwani hapo awali walikuwa wakibanana sana hali iliyokuwa ikiwajengea hofu ya kutofanya vizuri kitaaluma.
Akitoa neon la shukrani kwa niaba ya uongozi wa shule hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyanza Bw. Cliford Kassim ametoa shukrani kwa Kampuni ya AUMS, Mkuu wa Mkoa wa Geita, uongozi wa Halmashauri ya Mji Geita na kamati ya ujenzi kwa ushirikiano waliouonesha katika kuhakikisha madarasa yanakarabatiwa na kuleta maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Ukarabati wa majengo ya madarasa chakavu matano na Ofisi moja ya walimu umetekelezwa kwa ushirikiano wa pande mbili ambapo kamuni ya Afican Underground Services imechangia shilingi milioni 50 za kitanzania na Halmashauri ya mji Geita imetoa zaidi ya Shilingi Milioni 11 mpaka ukamilishaji.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa