Shule mpya ya Manga- Mkombozi wa watoto
Kukamilika kwa ujenzi wa Shule ya msingi Manga katika mtaa wa manga kata ya Mgusu, Halmashauri ya Mji wa Geita kumewawezesha watoto waliofikia umri wa kuanza shule wanaoishi katika mtaa huo na maeneo jirani kujiunga na masomo mwezi Januari 2019.
Shule hiyo yenye vyumba sita vya madarasa, ofisi ya walimu na choo cha wanafunzi chenye matundu 12, sita kwa wavulana na sita kwa wasichana imesajili wanafunzi 336 wa madarasa ya awali, la kwanza na la pili, ambapo madarasa yaliyopo kwa sasa yanatosheleza vyema idadi ya watoto walisajiliwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii alipotembelewa shuleni kwake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Ndugu Lugasia Nyatega ametoa shukrani za dhati kwa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kuona umuhimu wa kuwajengea shule watoto wa mtaa huo na kuwapongeza wananchi wa mtaa wa Manga kwa kujitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha wanafanikisha ujenzi wa shule hiyo yenye madhari na majengo yana yovutia.
Mwalimu Nyatega amesema kuwa changamoto ambayo wanakabiliana nayo kwa sasa ni uhaba wa walimu wa masomo ya awali, ambapo ameiomba idara ya Elimu msingi, Halmashauri ya Mji wa Geita kuangalia namna ya kuwapatia walimu wa masomo ya awali ili watoto wapate haki ya elimu kama inavyostahili.
Kwa upande wa Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Ndg. Yesse Kanyuma amesema kuwa amepokea ombi la walimu wa awali kutoka shule ya Msingi Manga na Ofisi yake inafanya utaratibu wa haraka kuhakikisha mwalimu mmoja wa masomo ya awali anahamishiwa shuleni hapo ili watoto waweze kufundishwa. Pia shule ya Msingi Manga itaendelea kupewa walimu katika vipindi tofauti pindi watakapopatikana.
Shule ya Msingi ni moja ya shule ambazo zimejengwa kwa asilimia kubwa na wananchi wa eneo husika baada ya wananchi hao kuelimishwa na kuhamasishwa kuchangia na kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo. Pia Halmashauri ya Mji imechangia shilingi milioni kumi zilizotumika kukamilisha ujenzi wa shule hiyo iliyofunguliwa rasmi Januari 7 mwaka 2019.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa