Shule Maalum Za Wasichana Kuongeza Wanasayansi
Ujenzi wa Shule maalum za wasichana ambazo zitadahili wanafunzi wa masomo ya sayansi pekee zimebainika kuongeza idadi ya wanafunzi hususan wa kike wa fani mbalimbali za sayansi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Mji wa Geita Mwalimu Rashid Muhaya alipokuwa akiongea na mwandishi wa Habari hii hivi karibuni Ofisini kwake alipokuwa akitoa ufafanuzi wa mapokezi ya fedha hizo na mikakati ya ujenzi wa shule hiyo ya Kitaifa ambayo itajengwa katika Kata ya Bombambili Geita mjini.
Mwalimu Muhaya ameeleza kuwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari( SEQUIP) imetoa fedha kwa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya bweni ya wasichana ya kitaifa kwa ajili ya masomo ya sayansi ikiwa na lengo la kuongeza fursa kwa wanafunzi wa kike kupata nafasi zaidi za kujiunga na masomo ya michepuo ya sayansi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Profesa Godius Kahyarara amewaagiza wataalamu wa Halmashauri kusimamia na kufanya ufuatiliaji wa ujenzi ipasavyo ili kuhakikisha ujenzi unakuwa bora na wenye kuzingatia thamani ya fedha itakayotumika. Pia wanatakiwa kufuata mwongozo wa ujenzi ipasavyo ili ujenzi wa miundombinu iliyopangwa ikamilike kabla au ifikapo mwezi Disemba 2023.
Kulingana na takwimu zilizopo katika Shule zinazopokea wanafunzi wa kike kwa kidato cha tano na sita zina uwezo wa kupokea wanafunzi 316 pekee, ambapo katika kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike katika michepuo ya sayansi Halmashauri ya Mji wa Geita imepatiwa Shilingi Bilioni tatu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujenga shule maalum ya wasichana ya masomo ya sayansi, ambapo mpaka ukamilishwaji wake itatumia kiasi cha Shilingi Bilioni nne za kitanzania.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa