Serikali Yawaonya Wanaojinufaisha Kupitia Makazi Ya Watoto
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa onyo kali kwa baadhi ya wamiliki wa makao ya Watoto ambao wanatumia usajili wanaopewa kwa maslahi yao binafsi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis alipofanya ziara ya kutembelea Kituo cha Watoto yatima na waliotelekezwa Moyo wa Huruma kilichopo Geita mjini na kuzungumza na Watoto pamoja na walezi wao hivi karibuni.
Mhe. Mwanaidi Khamis amesema kuwa kumekuwa na desturi ya baadhi wa wamiliki wa vituo vya Watoto kutumia picha za Watoto kwa maslahi yao binafsi ili kujipatia fedha au misaada mbalimbali kutoka kwa wafadhili na wahisani walioko ndani au nje ya nchi.
“Serikali haitawavumilia wamiliki wote wa makazi ya Watoto ambao watakiuka sheria na kanuni za uendeshaji wa vituo vya Watoto, bali endapo shirika lolote litathibitika kutumia Watoto kujinufaisha binafsi, shirika hilo litafutiwa usajili mara moja.” Ameongeza Mhe. Mwanaidi Khamis.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wanawake na makundi maalum ameeleza kuwa ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuona Watoto wa kitanzania hawapati tabu bali wanaishi katika mazingira salama. Pia ametoa pongezi kwa waanzilishi wa kituo cha malezi ya Watoto waliokosa fursa ya kulelewa majumbani kwa kuwalea Watoto hao kwa mapenzi makubwa kwani malezi ya Watoto yanahitaji moyo.
Mheshimiwa Mwanaidi Khamis amewashauri wanawake wote ambao hawajajiunga katika vikundi mbalimbali vinavyojishughulisha na kazi mbalimbali za kujiingizia kipato wameshauriwa kuunda vikundi hivyo ambavyo vitawawezesha kujikwamua kiuchumi kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Cornel Magembe amesema kuwa Halmashauri ya Mji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo likiwemo Jimbo Katoliki la Geita kuhakikisha Watoto wanaoishi katika makazi ya Moyo wa Huruma wanaendelea kupata huduma za msingi na kuishi kwa furaha, usalama na amani.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa