Serikali Yapongezwa Kwa Kukuza Uwekezaji
Mbunge wa Geita Mjini Mheshimiwa Costantine Kanyasu ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kujenga mazingira mazuri na wezeshi kwa wawekezaji hususan wa sekta ya madini ambao umewezesha kuvutia wawekezaji wengi wa madini katika Mkoa wa Geita kwa ujumla.
Pongezi hizo zimetolewa na Mbunge Kanyasu hivi karibuni alipokuwa akizungumza na washiriki wa kongamano la kujadili fursa za kiuchumi na uwekezaji zinazopatikana katika Mkoa wa Geita lililofanyika katika ukumbi wa Mkapa EPZA Bombambili Geita mjini hivi karibuni, ikiwa ni sehemu ya programu ya Maonesho ya sita ya kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mjini Geita.
Mhe. Kanyasu amesema kuwa uwekezaji mkubwa wa madini ya dhahabu unaofanywa na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi unaendelea kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo na ukuaji wa mji wa Geita kwa kasi kubwa.
“Sisi kama viongozi wa mji huu tumejipanga vyema kuhakikisha uwekezaji katika sekta ya madini ya dhahabu unakuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa fursa kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika mkoa wa Geita.” Aliongeza Mhe. Kanyasu.
Mbunge Kanyasu kupitia jukwaa hilo ameiomba Serikali kupitia Wizara ya madini kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zilizopo Geita likiwemo suala la vigingi na mipasuko linalotokana na wananchi kutolipwa fidia zao huku akimpongeza Waziri wa Madini wa awali Dkt. Doto Biteko kwa kuacha alama kubwa katika sekta ya madini.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita amesema kuwa wakurugenzi katika mkoa wa Geita wanaendelea kubainisha na kutenga maeneo ya uwekezaji ikiwemo kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Pia amewaahidi wachimbaji kutoachwa nyuma na fursa zilizopo katika mji wa Geita kwa sababu kipaumbele ni kwa watu wa Geita kwanza na baada ya hapo ni kwa watu wanaotoka nje ya mkoa.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa