Sekta Ya Madini Yazidi Kupaa Kiuchumi
Sekta ya Madini chini Tanzania imeendelea kukua zaidi na kuongeza pato laa Serikali katika miaka ya hivi karibuni. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mheshimiwa Angellah Kairuki wakati wa hafla ya ufungaji wa Maonesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye sekta ya Madini yaliyofanyika mjini Geita kuanzia Tarehe 17-27/9/2020 katika eneo maalum la uwekezaji kiuchumi Bombambili.
Mheshimiwa Kairuki amefafanua kuwa Sekta ya Madini imekuwa kwa kiwango kikubwa ambapo mwaka 2015 sekta hiyo ilikuwa ikichangia pato la Taifa kwa asilimia 3.4 lakini kwa sasa mchango wake umepanda hadi kufikia asilimia 5.2, kadhalika ametumia fursa hiyo kuwapongeza wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini kwa kulipa kodi kwa hiyari na kufanya kazi zao kwa kufuata sharia, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali.
Kwa upande wake Waziri wa Madini Mheshimiwa Dotto Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kutekeleza mipango ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija na kuwaboreshea mazingira yao ya kazi pamoja na kuwatengea maeneo yenye taarifa za kijiolojia ili kuepusha kuchimba kwa kubahatisha.
Mhe. Dotto Biteko pia ametoa wito kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa Madini kuyatumia Maonesho hayo kama chachu ya kuwahimiza kutumia teknolojia nafuu na zenye tija katika shughuli zao.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameeleza kuwa kwa mwaka 2020 dhahabu iliyopatikana katika Mkoa wa Geita ni zaidi ya tani tano yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 576 kutoka kwa wachimbaji wadogo. Haya ni mageuzi makubwa yaliyopatikana ndani ya Mkoa wa Geita katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano.
Maonesho ya Tatu ya Kimataifa katika Uwekezaji wa Teknolojia ya Madini yaliyofanyika kwa siku kumi katika Mkoa wa Geita yamehusisha washiriki mbalimbali zikiwemo Wizara mbalimbali, Mashirika ya Umma,Makampuni yanayojishughulisha na uchimbaji wa Madini, Taasisi mbalimbali za Serikali na Sekta binafsi, Umoja wa Wachimbaji wadogo Mkoa wa Geita(GEREMA) Taasisi za kifedha na wajasiriamali wadogo wanaofanya kazi kwa kushirikiana na Shirika la Viwanda vidogo vidogo( SIDO) kanda ya ziwa.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa