Rais Samia Kufanya Ziara Mkoani Geita
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi Mkoani Geita kwa siku mbili kuanzia tarehe 15 hadi 16/10/2022.
Akitoa taarifa kwa umma leo tarehe 13/10/2022 kwenye ukumbi wa ofisi yake mtaa wa Magogo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela amesema kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan atapokelewa wilayani Chato akitokea Mkoa wa Kagera na kufanya ziara ya kikazi katika wilaya za Chato, Geita na Bukombe kabla ya kuondoka kuelekea mkoani Kigoma.
Mhe. Shigela ameeleza kuwa baada ya Mhe. Rais kupokelewa atatembelea Hospitali ya kanda ya rufaa ya Chato ambapo atapokea taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo, kufahamishwa huduma zinazotolewa hapo na kuzindua hospitali hiyo. Baada yah apo Mhe. Rais akiwa njiani atasimama katika eneo la Buselesele na kuwasalimu wananchi wa eneo la Katoro na Buselesele na kisha kusafiri mpaka wilayani Geita.
Akiwa Wilayani Geita Mhe. Samia Suluhu Hassan atatembelea kituo kikubwa cha kupoozea umeme katika eneo la Mpomvu na kuzindua mradi huo kabla ya Kwenda kufungua rasmi kiwanda cha kusafisha Dhahabu Geita mjini na baada ya ufunguzi huo mchana wa tarehe 15 Oktoba atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara ambapo atawahutubia watanzania wote kupitia wananchi wa Mkoa wa Geita kwenye uwanja wa CCM Kalangalala.
Mkuu wa Mkoa wa Geita ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi ili kumlaki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni ziara yake ya kwanza Mkoani Geita tangu aingie madarakani pia kumshukuru kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi ya Zaidi ya shilingi Bilioni 190 ikiwemo ujenzi wa madarasa , mradi wa kusambaza umeme kwenye vijiji 132, mradi mkubwa wa maji kupitia ziwa Viktoria na mingine mingi katika sekta za Afya, barabara nk katika Mkoa wa Geita .
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan atahitimisha ziara yake mkoani Geita tarehe 16 Oktoba 2022 kwa kuwasalimia wananchi wa eneo la Runzewe wilayani Bukombe akiwa safarini kuelekea mkoani Kigoma.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa