Plan International Yaunga Mkono Mapambano Dhidi ya Corona
Shirika la Plan Inernational limeunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jitihada za kuhakikisha wanapambana kudhibiti maambukizo ya Virusi vya COVID-19. Shirika hilo limewezesha mafunzo juu ya namna ya kujikinga na Virusi vya COVID-19 kwa watu wenye ulemavu wapatao 100 kutoka Halmashauri mbili za Wilaya ya Geita Tarehe 16-17/4/2020 katika ukumbi wa Chuo cha Afya na Uuguzi Geita mjini.
Akizungumza kwa niaba ya shirika hilo Meneja Mradi Mkoa wa Geita Ndugu Adolf Kaindoa amesema kuwa Shirika la Plan kama wadau wa maendeleo katika Mkoa wa Geita walipata wazo la kuwaseminisha watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali kwa sababu wana haki ya kufahamu namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo wao binafsi pamoja na familia zao.
Ndg. Kaindoa ameongeza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya kuwajengea uelewa na ufahamu wananchi juu ya mbinu za kukabiliana na janga la Corona, pia njia nyingine zinazoendelea kutumika ni pamoja na vipeperushi, mabango yenye maelezo, matangazo kupitia vyombo vya habari vilivyoko ndani ya Mkoa lengo likiwa ni kuijengea jamii uelewa, utambuzi wa dalili za maambukizi na namna sahih za kujilinda na COVID-19.
“Katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 tutaendelea kushirikiana na Serikali kuimarisha ulinzi wa watoto, kupambana na vitendo vya unyanyasaji wa kijnsia, mimba zisizotarajiwa na ndoa za utotoni katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wako majumbani muda wote ikiwa ni jitihada ya Serikali kuzuia maambikizi ya ugonjwa wa Corona”. Aliongeza Adolf Kaindoa.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amelishukuru Shirika la Plan International kwa kufadhili mafunzo hayo kwa lengo la kuwapa elimu ya COVID-19 watu wenye ulemavu kwa kutambua kuwa virusi hivyo havibagui hali ya mtu. Pia kupitia mafunzo hayo tutaendelea kuzuia maambukizi mkoani Geita na hatimaye kupunguza au kumaliza kabisa kusambaa kwa virusi hivi nchi nzima.
Mhandisi Robert Gabriel ametumia fursa hiyo kuwasihi wakazi wa Mkoa wa Geita kutowaonea haya wageni wao kutoka Mikoa mingine ambao wana malengo ya kuwatembelea katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona wasitishe safari zao mpaka hali itakapokuwa shwari. Kadhalika ana imani kuwa washiriki wa mafunzo hayo wamepata elimu stahiki na uelewa mzuri juu ya virusi hivyo, njia sahihi za kujikinga, dalili za maambukizi na hatua stahiki za kuchukua ikiwa mtu atapata maambukizi.
Kwa upande wa watu wenye ulemavu, Mwenyekiti wa shirikisho la watu wenye ulemavu Mkoa wa Geita Bw. Robert Kinso ametoa shukrani za dhati kwa shirika la Plan International na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwakumbuka watu wenye ulemavu kwa sababu ni kundi ambalo mara kadhaa husahaulika kushirikishwa katika masuala muhimu yanayoendelea katika jamii. Pia ameomba elimu hiyo iwafikie wenzao walioko katika wilaya nyingine za Mkoa wa Geita licha ya wao pia kuahidi kufikisha elimu hiyo kwa wenzao ambao wana ulemavu wa kushindwa kutembea wala kutambaa pasipo msaada wa jamaa zao wa karibu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa