Ofisi ya LAPF Kanda ya Magharibi Yafunguliwa
Mfuko wa Jamii wa Serikali za Mitaa( LAPF) Tanzania umefungua rasmi ofisi yake ya kanda ya magharibi iliyoko katika Halmashauri ya Mji Geita Mkoani Geita.
Ofisi hiyo ya kanda ya magharibi itakayohudumia mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma pamoja na Halmashauri za Wilaya ya Sengerema na Buchosa zilizoko Mkoani Mwanza imefunguliwa katika Mkoa wa Geita ili kusogeza karibu kwa wanachama wa Mfuko wa LAPF walioko katika mikoa iliyoainishwa.
Akiongea katika hafla fupi ya ufunguzi wa Ofisi hiyo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) Mh. Joseph Sinkamba Kandege ameupongeza mfuko wa jamii wa LAPF kwa utendaji kazi mzuri na kuona umuhimu wa kufungua ofisi ya kanda ya magharibi katika Mkoa wa Geita.
Naibu Waziri huyo amesema kuwa Ofisi ya LAPF kanda ya magharibi itawapunguzia kero ya usafiri kwa umbali wa muda mrefu kwa wanachama waliokuwa wanasafiri kutoka Kigoma na Kagera kwenda katika Ofisi ya kanda ya ziwa Mkoani Mwanza kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali
Mh. Joseph S. Kandege ametoa wito kwa mifuko yote ya kijamii kuiga utaratibu mzuri unaofanywa na LAPF wa kulipa mafao ya kustaafu kabla ya muda wa kustaafu, utaratibu huu unawasaidia wastaafu kupanga mipango yao ya kimaisha mapema. Pia ameishauri mifuko hiyo kutoa elimu kwa wanachama wao juu ya umuhimu wa kujiandaa kwa maisha baada ya kukoma utumishi kuliko kujipanga kimaisha baada ya kupata fedha ya kiinua mgongo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI ameziagiza Halmashauri zote nchini ambazo zinadaiwa na LAPF pamoja na Mifuko mingine ya kijamii, michango ya watumishi wao hususani Watendaji wa Kata na Vijiji kuandaa utaratibu wa kuwasilisha michango ya watumishi hao na taarifa ya utekelezaji itumwe Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kuzichukulia hatua Halmashauri ambazo hazitatekeleza agizo hilo.
Akiwa Katika Halmashauri ya Mji Geita, Mh. Joseph S. Kandege alitembelea miradi mbalimbali inayoendelea kujengwa katika Mkoa wa Geita na Halmashauri ya Mji Geita ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Mkoa pamoja na ujenzi wa barabara, soko la kisasa na jengo la utawala la Halmashauri ya Mji Geita.
Sambamba na tukio la ufunguzi wa Ofisi ya kanda ya LAPF Mkoani Geita, LAPF wametoa mchango wa madawati 100 kwa Halmashauri ya Mji Geita ambapo Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga aliagiza madawati hayo yapelekwe katika Shule ya Msingi Nyantorotoro.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa