Mwenge Wa Uhuru Wazindua Klabu ya Tehama Nyankumbu Sekondari
Kiongozi wa Mbio maalum za Mwenge wa Uhuru 2021 Luteni Josephine P. Mwambashi amezindua rasmi klabu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu hivi karibuni wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Wilayani Geita.
Akizindua klabu hiyo ambayo ni mpya Kiongozi wa Mbio maalum za Mwenge wa Uhuru amewaasa wanachama na wanafunzi wasio wanachama kutumia Tehama kwa manufaa ya kujifunza masuala mbalimbali kwa urahisi zaidi na sio kufanya utapeli na kuangalia picha zilizo kinyume na maadili ya kitanzania.
“Tehama ni njia mahsusi ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo, wanafunzi mmepata fursa ya kujisomea vitabu na masuala mtambuka kupitia njia za kielektroniki. Kadhalika jamii nzima inakumbushwa kuitumia kwa usahihi na uwajibikaji ili iwasaidie watanzania katika sekta za biashara, elimu, kilimo na uvuvi.” Aliongeza Luteni Josephine Mwambashi.
Akiwa katika shule ya Sekondari ya wasichana Nyankumbu, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amezindua pia klabu ya wapinga rushwa na kuwakumbusha wanafunzi kuwa rushwa ni adui wa haki na kizuizi kikubwa katika kuleta maendeleo hivyo wanafunzi wana wajibu wa kuhakikisha kila mtanzania anashiriki kupambana na rushwa, wanafunzi wanatakiwa waendelee kutoa elimu katika jamii kwa sababu vijana ndio taifa la leo na nguvu kazi ya taifa pia wategemewa ambao wataongoza nchi miaka ya mbeleni.
Kikundi cha vijana cha Ufunuo ambacho kilipatiwa mkopo na Halmashauri ya Mji wa Geita na kununua magari matatu maarufu kama kirikuu kwa ajili ya biashara ya kusafirishia mizigo wamepongezwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge kwa kutoona ulemavu kama ugonjwa na kukaa bure majumbani, bali wao wametumia fursa iliyotolewa na Serikali kujikwamua wao binafsi na familia zao.
Mwenge wa Uhuru pia umezindua shamba la miti lenye ukubwa wa hekta 25 lililomea miti 27,700 mali ya Ndugu Paul Kyando. Akizungumza baada ya uzinduzi wa shamba hilo kiongozi wa Mbio maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 amempongeza mkulima huyo kwa kuajiri vijana 40 katika shamba lake na kuongeza kuwa uwepo wa shamba hilo unasaidia uhifadhi wa mazingira na itakapovunwa itasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri.
Ukiwa Wilayani Geita Mwenge wa Uhuru 2021 uliobeba ujumbe mkuu usemao ‘ TEHAMA NI MSINGI WA TAIFA ENDELEVU; ITUMIE KWA USAHIHI NA UWAJIBIKAJI’ umekimbia umbali wa kilomita 85.2 na kufungua, kuzindua na kutembelea miradi 11 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 11.5, Miradi mingine iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru ni Pamoja na Shule ya Msingi Uwanja, Barabara ya Madini- KKKT, Kikundi cha vijana Safina, Barabara ya Upendo Dispensary- American chips, Hospitali ya Wilaya Katoro, Mradi wa maji Katoro na Klabu ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya Shule ya Sekondari Geita.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa