Mwenge Wa Uhuru 2023 Wafungua Shule ya Msingi Juhudi
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Ndugu Abdalla S. Kaim amefungua rasmi Shule mpya ya Msingi Juhudi iliyoko katika Mtaa wa Mwatulole kata ya Buhalahala wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Mji Geita hivi karibuni.
Ndugu Kaim ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuwaagiza walimu na wanafunzi kuhakikisha miundombinu iliyojengwa inatunzwa vyema kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 kadhalika ametoa pongezi za dhati kwa Halmashauri ya Mji Geita kwa kutumia fedha za mapato ya ndani kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Pia wazazi na walezi mjini Geita wamepongezwa kwa kujitahidi kuienzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru kwa kuwaruhusu Watoto kushiriki katika shughuli ya kuulaki Mwenge wa Uhuru ulipokimbizwa katika maeneo mbalimbali Geita mjini,
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwatulole Bi. Catherine Mugusi ameeleza kuwa Shule ya Msingi Juhudi ambayo imejengwa kwa shilingi milioni 987.6 ambapo Halmashauri ya Mji Geita imechangia Shilingi milioni 130, Serikali kuu Shilingi milioni 800, nguvu za wananchi milioni 1.8 na mradi wa GPE-LANES Shilingi milioni 55.8
Bi. Mugusi ameongeza kuwa kukamilika kwa Shule mpya ya Msingi Juhudi kutanufaisha jumla ya wanafunzi 995 na kupunguza msongamano katika shule za Msingi Nguzombili na Mwatulole ambazo kwa sasa zina jumla ya wanafunzi 9,649. Pia utasaidia kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Mwenge wa Uhuru 2023 ulizindua, kufungua, Kuwekewa jiwe la msingi na kutembelea miradi 12 yenye thamani ya shilingi Bilioni 4.02 katika maeneo mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Mji Geita. Kauli Mbiu ya Mwaka 2023 inasema “ Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na kwa uchumi wa Taifa.”
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa