WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, amewahimiza watafuta fursa za uwekezaji wazingatie kuwekeza kwenye maeneo yenye uhakika wa kupata malighafi na soko, na moja ya eneo hilo ni mkoa wa Geita.
Waziri Mwakyembe aliyasema hayo jana wakati akifungua Jukwaa la Fursa za Biashara Geita lililofanyika jana mjini Geita. Jukwaa hilo lilianza juzi kwa maonesho ya bidhaa zinazozalishwa hapa Geita.
“Ni vyema wawekezaji wazingatie kwamba viwanda havitafanya vizuri sana kama havitapata malighafi katika eneo husika. Geita ina fursa nzuri ya kuwa na viwanda vinavyotegemea mazao ya migodi, samaki, kilimo na mifugo,” alisema
Alisema Geita pia ina fursa ya soko kutokana na jiografia yake kwa kupakana au kuingiliwa karibu na nchi nyingi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Nimedokezwa hapa kwamba kwa sasa sato wanaovuliwa Geita ni wakubwa na wengi. Katika hali hiyo ni kwa nini Geita isiwe na kiwanda cha kusindika minofu ya samaki?” alihoji.
Aliwaambia washiriki takribani 400 waliohudhuria katika jukwaa hilo kukumbuka kwamba ujio wa wadau mbalimbali wa maendeleo kwenye jukwa hilo vikiwemo vyombo kadhaa vya fedha ni kwa sababu wanajua Geita kuna fursa.
“Ukiona wadau wengi wamekuja hapa Geita basi jua kwamba wameshagundua fursa zilizopo Geita na hivyo wamekuja kujitambulisha na kuwa tayari kutumia fursa inayopatikana Geita,” alisema Waziri Mwakyembe. Alisema Jukwaa hilo lililofanyika jana ni nafasi nzuri kuieleza dunia yale yanayopatikana Geita na pia kuwawezesha wana Geita kujenga uhusiano mpya na wadau mbalimbali.
Dk Mwakyembe alitoa pongezi kwa uongozi wa TSN kwa kutangaza vyema Jukwaa la Biashara na kuwafanya Watanzania na watu wengine katika Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla kujua yanayoendelea hapa Geita.
Alisema majukwaa ya biashara yako bega kwa bega na dira ya nchi yetu ya kuipeleka nchi katika uchumi wa kati.
“Lengo kubwa la majukwa haya ni kuamsha ari ya wafanyabiashara na wawekezaji katika kuitikia wito wa Rais John Magufuli ya kufanya nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel alikaribisha wawekezaji katika mkoa wake akisema wamejipanga kuhakikisha kwamba mwekezaji yeyote anayekuja Geita hazungushwi wala kuomba rushwa.
“Geita ni mkoa rafiki kwa mwekezaji. Hapa tumekataa urasimu, na hakuna kuzungushwa. Anayetaka kuwekeza Geita tunamshughulikia kwa siku chache tu. Tuko wakali sana kwa mwekezaji anayezungushwa hata siku moja tu.
“Urasimu, kuzingushwa zungushwa na kuombana rushwa hapa Geita tunaita zilipendwa… Kwenye rushwa hata maua yanakauka, rushwa inazuia mkoa kunyanyuka,” alisema.
Mkuu wa mkoa alisema kutokana na jiografia yake Geita ni sehemu nzuri ya kuwekeza kuliko maeneo mengi ya Afrika Mashariki
Aliufafanisha mkoa wake na nchi ya ahadi akisema karibu kila kitu kinachoelezwa katika vitabu kuhusu nchi ya ahadi vinapatikana Geita.
Aliongeza: “Geita Mungu alishaifanya kuwa tajiri, tunachoomba sasa ni Mungu atupe jicho la kuona raslimali tuliyo nayo na kuisimamia vyema,” alisema
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa