MRADI WA SEQUIP KUWAKOMBOA WANAFUNZI ZAIDI YA 180 GEITA
“Tunasoma kwa taabu, mvua hutunyeshea, jua kutuwakia, tunakimbizwa na wanyama wakali kama fisi, dada zetu wanakumbana na vishawishi kutoka kwa vijana wawapo njiani kuelekea nyumbani na kikubwa Zaidi tunafika majumbani tukiwa tumechoka sana na kushindwa kujisomea muda wa ziada.” Kauli ya Joseph Mwebeya mmoja wa wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Sekondari Bulela akitokea kata jirani ya Shiloleli.
Mayala Samike, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Bulela ni miongoni mwa wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kufika shuleni, ambaye amesema kushinda na njaa Pamoja na kukosa vipindi vya kwanza darasani imekuwa sehemu ya Maisha yao hali inayopelekea kuzorota kwa uwezo wake kitaaluma kwani wakirejea nyumbani baada ya masomo wanakuwa na uchovu ambao huwalazimu kulala na kushindwa kupata muda wa kujisomea.
Kukamilika kwa ujenzi wa Shule mpya ya kwanza ya Sekondari katika kata ya Shiloleli Halmashauri ya Mji wa Geita ambayo iko katika hatua za ukamilishwaji kupitia mradi wa SEQUIP kutoka Serikali kuu kutawatatulia changamoto ya kutembea umbali wa kilomita 16 kwa safari moja wanafunzi wa kata hiyo ambao kwa sasa wanakwenda kupata masomo yao katika Shule ya Sekondari Bulela iliyoko kata ya Jirani.
Akizungumza na mwandishi wa Habari hii hivi karibuni, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Bulela Mwalimu Pelicia Ponsian ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwakumbuka wanafunzi wa Shiloleli na kuona umuhimu wa kupata shule katika mazingira yao.
Mwalimu Ponsian amesema kuwa uwepo wa shule hiyo mpya utawasaidia wanafunzi wanaotaraji kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023 pamoja na wanafunzi 183 wanaosoma katika shule yake wanaotoka kata ya Shiloleli ambapo wanatembea umbali mrefu na wakati mwingine hususan kipindi cha masika wanakwama kufika shuleni au kufika shule kwa kuchelewa na kukuta masomo yameshaanza kufundishwa.
Mwalimu Ponsian ameongeza kuwa changamoto nyingine ni matokeo ya wanafunzi hao yamekuwa si ya kuridhisha kwa sababu uelewa wao darasani hupungua kutokana na uchovu wa safari ya kutoka nyumbani hadi shule, kushinda njaa, utoro wa rejareja ambao husababishwa na sababu zilizo nje ya uwezo wa wanafunzi kama uwepo wa wanyama wakali na vibaka kwenye mapori wakati wa kwenda shuleni.
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Shiloleli Mhe. Boniphace Kaswahili Fulano amesema yeye ameunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa bure eneo lake lenye Zaidi ya ekari tisa ili shule ya Sekondari ya kwanza iweze kujengwa na kuwanufaisha Watoto wa kata hiyo. Pia ametoa wito kwa wazazi kuwahamasisha Watoto kupenda shule kwani elimu ndiyo ufunguo wa Maisha.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji Geita Ndugu Rashid Muhaya amesema kuwa kutokana na changamoto ya mdondoko wa wanafunzi inayosababishwa na umbali mrefu katika bajeti ya mwaka 2022/2023 Halmashauri imelenga kujenga shule mpya nne katika kata mbalimbali ambazo zitagharimu Shilingi Bilioni 1.07
Shule mpya ya Sekondari katika Kata ya Shiloleli ni miongoni mwa shule mpya 11 za Sekondari zilizojengwa katika Halmashauri ya Mji Geita kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufika shule kwa baadhi ya wanafunzi wanaotumia muda mwingi kutembea mpaka shuleni kwa ajili ya masomo.
“Ndani ya miaka mitatu iliyopita Halmashauri ya Mji wa Geita tumefanikiwa kujenga shule 11 za sekondari ambazo kwa kiasi zimesaidia kupunguza changamoto ya wanafunzi ambao hutembea umbali mrefu na kuondoa msongamano wa wanafunzi darasani.” Aliongeza Ndg. Muhaya.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mradi wa kuboresha elimu wa SEQUIP imetoa kiasi cha shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ili kuwanusuru wanafunzi wanaotembea umbali wa kilomita 18 hadi 32 kwenda shule na kurudi nyumbani. Mpaka sasa Halmashauri ya Mji Geita ina shule za 19 za sekondari ambapo wanafunzi wa shule sita wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda na kukudi shule.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa