Mradi wa Ufundi kuwakwamua vijana kiuchumi
Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM)umeikabidhi Serikali ya Mkoa wa Geita Mradi wa Chuo cha ufundi kitakachowawezesha wanawake na vijana kujiajiri na kujikwamua kiuchumi na kijamii kuanzia ngazi ya familia na Taifa kwa ujumla.
Akiongea wakati wa hafla fupi ya makabidhiano hayo hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameishukuru GGM kwa kuwa sehemu ya maendeleo ya Mkoa kwa kutambua umuhimu wa wananchi wanaoizunguka kampuni yao kuwa na shughuli zitakazowawezesha vijana na wanawake kujikwamua kiuchumi kupitia fani mbalimbali zilizopo katika chuo hicho.
Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa mradi huo utakuwa ni chanzo cha ongezeko la viwanda katika mkoa wa Geita kwani fani kama ushonaji, ufyatuaji wa matofali, uchomeleaji, utengenezaji magari utatoa fursa kwa wakufunzi wa chuo hicho kuanzisha miradi au viwanda vyao binafsi vitakavyowawezesha wao na jamii nzima.
“Serikali itauenzi mradi huu ambao ni mkubwa ulioanzishwa na kampuni ya GGM, nia ya Mkoa wa Geita ni kupanua ajira kwa vijana na wanawake hivyo uwekezaji kama huu unahitaji matunzo, na katika kuhakikisha matunzo hayo yanapatikana nawaagiza watendaji wa Halmashauri ya Mji Geita wanaohusika na masuala ya ufuatiliaji vikundi kuvilea na kuvitembelea vikundi vilivyopo katika chuo hicho mpaka vitakapokomaa na kuiwezesha Serikali pia kupata mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa watakazozitengeza.” Aliongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Kwa upande wa Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita, Meneja Mahusiano wa Mgodi Ndg. Manase Ndoroma amesema kuwa mradi huo ambao umegharimu kiasi zaidi ya shilingi Bilioni mbili za kitanzania ulikamilika mwaka 2015 na wameukabidhi mikononi mwa Serikali wakiwa na Imani kuwa wanufaika waliofanya kazi katika mradi huo tangu ulipoanza wameweza kuongeza ujuzi katika fani zao.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa