Mradi Wa BOOST Kupunguza Msongamano wa Wanafunzi
Halmashauri ya Mji wa Geita inatarajia kujenga shule mbili mpya za msingi kupitia mradi wa kuimarisha na kuboresha elimu ya awali na msingi (BOOST) kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo, Kaimu mratibu wa BOOST Bi. Rahel Mwera ameeleza kuwa Halmashauri ya Mji Geita inatarajia kupokea Shilingi 1,080,600,000/= ambazo zitatumika katika ujenzi wa shule mbili mpya za msingi katika kata ya Buhalahala.
Bi. Rahel Mwera ameeleza kuwa shule hizo mpya zitajengwa katika mtaa wa Mwatulole ambako baada ya uchambuzi wa tathimini ya mahitaji na hali ya miundombinu ya shule za msingi katika Halmashauri zote 184 nchini Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa ilibaini kuelemewa kwa shule za msingi Mwatulole na Ngunzombili kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi isiyowiana na idadi ya madarasa yaliyopo kwa sasa.
Kupitia mradi wa BOOST Halmashauri ya Mji Geita inatarajia kupokea Shilingi 1,653,300,000/= itajenga vyumba 18 vya madarasa katika shule tofauti, madarasa mawili ya mfano kwa elimu ya awali, chumba kimoja cha darasa la elimu maalum na matundu 13 ya vyoo.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa maagizo kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha zinazotolewa katika utekelezaji wa miradi hiyo zinakamilisha ujenzi kama ilivyopangwa ili kuepusha miradi mingi kutokamilika huku fedha zikiwa zimekwisha. Pia thamani ya fedha itakayotolewa iendane na majengo yatakayojengwa ili kufikia matokeo yaliyokubalika.
Mradi wa BOOST utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021/2022 hadi 2025/2026 ambapo utatekelezwa kwa awamu tofauti. Mkoa wa Geita utapokea Shilingi 9,781,100,000 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 11, vyumba vya madarasa 143 ya Shule za Msingi, vyumba vya madarasa ya mfano ya Elimu ya Awali 12, chumba kimoja cha darasa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum na matundu 94 ya vyoo.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa