MPANGO WA TPRP KUNUFAISHA WANANCHI GEITA
Kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya elimu ambayo iko katika hatua ya ukamilishwaji kupitia Mpango wa kupunguza Umaskini Tanzania (TPRP) inayotekelezwa kwa ushirikiano wa Halmashauri ya Mji wa Geita na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini( TASAF) kutawanufaisha wananchi waishio katika mitaa ya Nyanza, Bombambili, Kivukoni, Mwatulole na Shinde.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji Geita Ndugu Upendo Kilonge wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo iliyofanywa na wajumbe wa Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Mji wa Geita hivi karibuni.
Ndg. Upendo Kilonge amefafanua kuwa mwezi machi 2022 Halmashauri yake ilipokea Shilingi 411,307,414.58 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya shule na wanajamii walioko kwenye maeneo ya utekelezaji wa miradi wamechangia kiasi cha shilingi 25,159,519 kwa lengo la kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuwasaidia wanafunzi, walimu na jamii kwa ujumla.
“Miradi inayotekelezwa kupitia mpango wa TPRP ni Ujenzi wa jengo la utawala Shule ya Sekondari Nyanza, Ujenzi wa bweni la wavulana katika shule ya Sekondari Mwatulole, Ujenzi wa jengo la utawala Shule ya Sekondari Bombambili, Ujenzi wa madarasa mawili, ofisi moja ya walimu na choo cha matundu sita katika Shule ya msingi Kivukoni ambapo mpaka sasa miradi yote imetumia kiasi cha shilingi 394,024,011.10”. Aliongeza Ndg. Upendo Kilonge.
Ndugu Kilonge ameeleza kuwa ujenzi wa miradi hiyo inatekelezwa kwa kutumia mafundi wa jamii( local fundi) kwa kushirikiana na wananchi wa ngazi zote chini ya usimamizi wa kamati maalum( CMC) ngazi ya jamii ambao wamepatiwa mafunzo, wawezeshaji kutoka Halmashauri ya Mji Geita na timu ya wataalam kutoka TASAF.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwatulole Bi.Roseline Mariki amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa bweni la wavulana katika shule yake kutawawezesha wanafunzi 80 wa kidato cha tano na sita kutoka katika mikoa mbalimbali kupata fursa ya kuishi bwenini na kupata muda mwingi wa kujisomea.
Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji Geita amewasihi wananchi kujitoa kwa muda muafaka katika kushiriki kikamilifu katika kazi zote zinazowahusu ili kuweza kumaliza kazi kwa wakati, kadhalika kamati zinazohusika na usimamizi, manunuzi na mapokezi zishiriki kikamilifu katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mwongozo wa usimamizi miradi ili kuwezesha miradi hiyo kukamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa