Mpango Kabambe 2017-2037 kubadili Mandhari ya Mji Geita
Kuzinduliwa kwa Mpango Kabambe wa Mji wa Geita(Geita Town Master Plan) kutawezesha kupanga matumizi ya ardhi kwa ujumla na kukuza fursa za uwekezaji, biashara ,uchumi, utawala, maendeleo ya jamii na kulinda mazingira kwa kipindi cha miaka 20.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya makazi Mheshimiwa Angelina Mabula alipokuwa akiongea na wadau mbalimbali wa maendeleo mjini Geita hivi karibuni wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa mpango kabambe katika ukumbi wa Gedeco Geita mjini.
Mhe. Angelina Mabula ametoa pongezi za dhati kwa uongozi wa Halmashauri ya Mji Geita kwa uandaaji wa mpango kabambe ambapo amefurahishwa kuona namna kila kiongozi hususan wa siasa wanauelewa vyema mpango wao utakaowawezesha kuuendeleza mji na kudhibiti matumizi ya ardhi yasiyofaa.
Naibu Waziri wa Ardhi alitumia fursa hiyo kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita kuweka wasimamizi watakaofanya kazi ya kupitia mara kwa mara kusimamia udhibiti wa ujenzi holela na uvamizi wa maeneo ambayo yameainishwa kwenye mpango kabambe. Kadhalika ametoa rai kwa watumishi wa idara ya ardhi kuhakikisha wanautendea haki mpango kabambe kwa kutopokea maombi ya kubadili mpango wa matumizi ya ardhi usio na tija kwa matashi ya mtu binafsi au kundi la watu Fulani.
Kwa upande wake Mbunge wa Geita mjini Mheshimiwa Costantine Kanyasu amesema kuwa tukio la uzinduzi wa mpango kabambe ni njia ya kuelekea kwenye ndoto ya kuwa manispaa naimani yake juu ya wananchi wa Geita ni kuwa watauishi mpango kabambe huo kwa kutokujenga katika maeneo ambayo yameshaainishwa kwa ajili ya miradi ya huduma za kijamii kama barabara za juu na mengineyo.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mheshimiwa Joseph Lugaila ametoa rai kwa wadau wote wa maendeleo mjini Geita kushirikiana kikamilifu na uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita katika kuhakikisha lengo la kuupanga mji wa Geita katika viwango vinavyotakiwa tofauti na hali ilivyo kwa sasa linafanikishwa kwa asilimia mia moja na zaidi.
Mpango kabambe uliozinduliwa utakuwa na faida mbalimbali ambazo ni kuondoa migogoro ya ardhi inayotokana na mwingiliano wa kimatumizi, kutoa fursa za kiuwekezaji kwa viwanda na biashara, kuwa na mji uliopangwa wenye makazi bora, kuhifadhi na kulinda mazingira na kutoa fursa za ujenzi wa miundombinu na huduma za kijamii.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa