Miongozo Ya Elimu Itumike Kuboresha Taaluma – DC
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mheshimiwa Wilson Shimo amewaagiza wataalam wa idara za elimu wakiwemo walimu wote katika Halmashauri ya Mji wa Geita kuhakikisha wanaitumia vyema miongozo ya uboreshaji elimu iliyotolewa na Serikali kwa kuboresha taaluma kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, pia kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu katika wilaya ya Geita.
Mhe. Shimo ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akiongea na walimu baada ya kuzindua rasmi miongozo ya uboreshaji wa elimu ya Msingi na Sekondari kwa Halmashauri ya Mji wa Geita, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Nyankumbu
Mkuu wa Wilaya ya Geita amewaeleza walimu kuwa watambue kuwa wao ndio wenye wajibu wa kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizoko katika maeneo yao ya kazi, hivyo miongozo iliyotolewa imepitia na kutafuta ufumbuzi wa baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya elimu na walimu kwa ujumla.
“Ndugu zangu walimu ongezeni mbinu shirikishi za kufundisha ili wanafunzi wapate uelewa zaidi. Pia wazazi na walimu toeni mikakati ya kuzuia utoro sugu na rejareja kwa wanafunzi kwa ushirikiano na mashirika mbalimbali na Taasisi za umma zinazoshughulikia masuala ya elimu na haki za watoto, Kwa sababu utoro ni moja ya kizuizi kikubwa katika maendeleo ya wanafunzi kitaaluma na kinidhamu”. Aliongeza DC Shimo.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhe. Johhn Lunyaba Mapesa Diwani wa Kata ya Nyankumbu amewaasa walimu kuwa suala la kutumika vema kwa miongozo ya elimu lichukuliwe katika uzito unaostahili ili Halmashauri iweze kuvuka kutoka ilipo na kwenda juu zaidi kitaaluma. Kadhalika Mhe. Lunyaba amewakumbusha walimu hasa wa shule za msingi kuzitendea haki nafasi walizopewa ili kuhakikisha shule zote ndani ya Mji wa Gieta zinakuwa nafasi ya juu.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa imeandaa miongozo baada ya kubaini uwepo wa changamoto mbalimbali na kuainisha hatua zinazotakiwa kuchukuliwa ili kukabiliana nazo kwa kushirikiana na wasimamizi wa elimu, wazazi/walimu, jamii, viongozi na wadau mbalimbali katika ngazi zote za usimamizi wa sekta ya elimu
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa