MILIONI 605 KUTOKA GEITA MJI ZANUFAISHA VIKUNDI
Jumla ya vikundi 67 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kutoka katika kata mbalimbali za Halmashauri ya Mji wa Geita vimepatiwa mkopo wa Shilingi milioni 605 kwa ajili ya kuviwezesha kutekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi ambapo shilingi 449,000,000 zinatokana na asilimia 10% ya makusanyo ya ndani ya halmashauri na Shilingi 156,000,000/=ni marejesho ya mikopo.
Akitoa mchanganuo wa Shilingi 372,118,000 zilizotolewa kwa vikundi 20 vya vijana, Shilingi 219,882,000 vikundi 45 vya wanawake na Shilingi 13,000,000 vikundi 2 vya watu wenye ulemavu wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika tarehe 18/7/2022 Geita mjini, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Bi. Zahara Michuzi amesema kuwa katika fedha iliyotolewa shilingi 192,800,000/= zimetumika kununua bajaji 21 na pikipiki moja ambazo zimegawiwa kwa vijana wa umoja wa waendesha bajaji mkoa wa Geita.
Bi. Zahara Michuzi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuendeleza progamu hii ya uwezeshaji wa makundi haya maalum kwani imesaidia kupunguza kero nyingi zilizokuwa zinawakabili wajasiriamali wengi kama ukosefu wa mitaji, wanawake kuondokana na utegemezi kutoka kwa waume zao hali iliyosababisha kuongezeka upendo katika familia na kuongezeka kwa uchumi binafsi wa wanufaika na jamii kwa ujumla.
Akikabidhi hundi na bajaji hizo mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Geita Ndg. Janeth Mobe ameipongeza Halmashauri ya Mji kwa kuendelea kutoa mikopo isiyokuwa na riba kwa makundi maalum na kuwataka wanavikundi kufanya shughuli za uzalishaji mali na kutochukulia fedha hizo kama hisani au sadaka bali wanapaswa kuzirejesha kwa wakati kwa mujibu wa sheria.
“Pamoja na mafanikio mengi mnayoyapata nitumie nafasi hii kuwasihi kuzitunza bajaji na pikipiki mlizokabidhiwa leo ili ziweze kudumu na pia madereva zingatieni sheria za barabarani kwa kuendesha vyombo vyenu kistarabu, kutoruhusu vyombo vyenu vya usafirishaji kutumika katika matukio ya kihalifu kama wizi, ujambazi, magendo nk. Mkionyesha weledi katika shughuli zenu mtakuwa mnaunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vitendo.
Akizungumza kwa niaba ya wanavikundi walionufaika na mkopo huo, Bi. Riziki Ramadhani ambaye ni dreva wa kike pekee wa bajaji ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na halmashauri ya Mji wa Geita kwa kuendelea kuthamini mahitaji ya makundi maalum jitihada zao za kujikwamua kiuchumi kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba . Pia amewasihi wenzake hususan wanawake kufanya kazi zote halali pasipo kuogopa kuchekwa au kubezwa na mtu yeyote.
Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Mji Geita ilitenga Shilingi 909,574,000 kutoka kwenye mapato ya ndani ambazo fedha hizo zimekopeshwa kwa vikundi 115 vya wajasiriamali na katika mwaka huo wa fedha kiasi cha shilingi 658,816,000 kimerejeshwa kutoka kwenye vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa