Milioni 50 za CSR Zawezesha Upatikanaji wa Zahanati
Jumla ya Shilingi Milioni 50 za kitanzania zimetolewa na Halmashauri ya Mji wa Geita kupitia fedha za CSR ili kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Magereza katika kata ya Kalangalala Geita Mjini.
Akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la zahanati hiyo tarehe 18/11/2019 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mheshimiwa Leonard Bugomola amesema kuwa Halmashauri yake kupitia fedha ya CSR inayotolewa na Mgodi wa Dhahabu iliamua kuweka nguvu kwenye ujenzi wa zahanati ya Magereza kwa lengo la kuhudumia wafungwa, mahabusu na wananchi wa mitaa ya jirani.
Mheshimiwa Zephania Mahushi ambaye ni Diwani wa Kata ya Kalangalala amewataka wananchi wote wanaoishi katika mitaa iliyo jirani na gereza la Geita mjini kutumia huduma zitakazotolewa na zahanati hiyo kwa gharama nafuu na karibu na nyumbani.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza Kampuni ya GGM kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutekeleza miradi ya kimkakati yenye matokeo chanya katika mji wa Geits kupitia mpango wa fedha za uwajibikaji wa Kampuni kwa jamii( CSR).
“Kwa muda mrefu tumekuwa na changamoto ya wagonjwa katika gereza letu kukabiliwa na magonjwa mbalimbali lakini kwa msaada wa ujenzi huu wa ujenzi wa zahanati na mabweni, sasa tuna uhakika kwamba ripoti za magonjwa ndani ya magereza na maeneo yanayozunguka magereza zitapungua baada ya kukamilika kwa mradi huu. Naushukuru Mgodi wa Dhahabu wa Geita kwa kutoa vifaa vya ujenzi ambavyo vimetumiwa ipasavyo na wafungwa stadi waliokamilisha kazi nzuri ya ujenzi wa mradi huu.” Aliongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amewapongea GGM kwa kuona umuhimu wa madini wanayozalisha kuwanufaisha watanzania ili siku mgodi utakapofungwa wananchi wabaki na miradi itakayowanufaisha.
Waziri wa Madini amempongeza Mkuu wa Gereza la Geita kwa kuguswa na hali halisi ya wafungwa na wananchi wanaowazunguka juu ya uhitaji wa huduma ya afya na kuamua kuanzisha ujenzi wa zahanati. Pia amewasihi wananchi kuitunza vizuri zahanati hiyo ili iweze kudumu na kutoa huduma kwa watu wengi zaidi hadi vizazi vijavyo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita Bw. Richard Jordinson amesema GGM ni kampuni Raia nchini Tanzania itaendelea kusaidia jamii jamii inayozunguka mgodi huo na zahanati hiyo ni ushahidi Dhahiri kwamba GGM, Serikali na jamii zinaweza kufanya kazi kwa pamoja katika kuboresha maisha ya watu kupitia uwekezaji wa miundombinu ya kijamii na huduma.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa