Migodi ya Madini Nchini Yaagizwa Kuchangia Huduma za Jamii
Waziri wa Madini Mheshimiwa Dotto Biteko ameagiza kampuni zote zinazojishughulisha na uchimbaji madini kuhakikisha wanatekeleza sheria ya uwajibikaji wa kampuni kwajamii kwa kuchangia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo wanayofanyia kazi.
Mhe. Dotto Biteko ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa Dhahabu katika Soko kuu la Dhahabu Geita mjini hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kukagua majengo ya Maduka awamu ya pili na tatu ambayo yamejengwa kupitia fedha za uwajibikaji wa migodi kwa jamii( CSR) kutoka mgodi wa Dhahabu wa Geita( GGM).
Waziri wa Madini ametoa shukrani kwa wafanyabiashara wote wa Dhahabu nchi nzima kwa kuivika nguo Serikali kwa kupandisha kiwango cha ukusanyaji ambacho hakijawahi kutokea ambapo Mwezi Mei Wizara ya Madini imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 479.9
Aidha Mhe. Biteko amekemea tozo zisizo za lazima kwa wachimbaji wadogo ambazo zinatozwa na baadhi ya wamiliki wa leseni na Serikali za vijiji ilhali Serikali ilishaondoa tozo nyingine zisizo za lazima ili kuepusha utoroshwaji wa madini. “Wizara imesimamia vyema wachimbaji wadogo licha ya kuwepo kwa changamoto za ukusanyaji wa kodi kwa mwaka huu kwa sababu ya kushuka kwa uzalishaji kutokana na kunyesha kwa mvua nyingi.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita( GGM) Ndg. Simon Shayo amesema wamejipanga kuhudumia jamii kwa kujenga soko la wajasiriamali hali ambayo itaongeza kipato kwa kina mama wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo . Pia kampuni yake imetenga Shilingi Bilioni 5.5 kwa ajili ya huduma mbalimbali za kijamii.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa kupitia sekta ya madini kuna mabadiliko makubwa ya maendeleo mkoani Geita zikiwemo huduma mbalimbali za kijamii zinazoboreshwa hususan huduma za afya, elimu na masoko ya kisasa kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini.
Wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Mji Geita Mhe. Dotto Biteko alitembelea na kukagua miradi mingine inayotekelezwa kupitia fedha za CSR kama ujenzi wa soko la wafanyabiashara Katundu, ujenzi wa jengo la utawala katika eneo maalum la uwekezaji kiuchumi na kiwanda cha kusafisha Dhahabu Geita ambapo ujenzi wa miradi yote bado unaendelea.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa