NAIBU WAZIRI Ofisi ya Rais TAMISEMI (Elimu), Mhe. Zainab Katimba ametoa rai kwa wanafunzi wote nchini kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kufaulu kwa viwango vya juu ili badae walitumikie taifa.
Mhe.Katimba ametoa rai hiyo alipotembelea shule mpya maalum ya wasichana ya sayansi iliyopo Halmashauri ya Mji Geita Mkoa wa Geita kwa lengo la kukagua miundombinu iliyojengwa na kujionea maboresho yaliyofanywa na serikali katika ujifunzaji na ufundishaji kwenye sekta ya elimu nchini.
Amesema kuwa dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha watanzania wanapata elimu iliyobora katika mazingira mazuri hivyo ni wajibu wa wanafunzi kusoma kwa bidii ili kutimiza malengo yao.
Akitoa taarifa ya elimu Mkoa wa Geita, Katibu Tawala Mkoa huo, Mohamed Gombati amesema kwa upande wa shule ya sekondari ya wasichana imepokea Sh bilioni 3 katika awamu ya kwanza na Juni mwaka huu zimepokelewa Sh bilioni 1.1 kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya majengo na tayari imeshaanza kuchukua wanafunzi.
Amesema kwa mwaka 2021/22 Mkoa wa Geita ilipokea Sh bilioni 17, mwaka 2022/23 zilipokelewa Sh bilioni 31 na kwa mwaka 2023/24 zilipokelewa Sh bilioni 32 bila kujumuisha fedha zinazotolewa kugharamia elimu bila ada.
Amesema kuwa katika fedha za ndani zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo za asilimia 60 au 40 kiwango kikubwa kinaelekezwa kwenye sekta ya elimu.
Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya sayansi ya Mkoa wa Geita, Mwamin Kagoma amesema shule hiyo imegharimu Sh bilioni 4 na mpaka sasa wanafunzi 172 kati ya 211 waliopangiwa kujiunga na kidato cha tano wameripoti shuleni.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa