Mgusu Wajivunia Mema Ya Serikali ya Awamu ya Tano
Maendeleo katika sekta za elimu, afya , utawala bora na nishati ya umeme wa uhakika yanayopatikana katika Kata ya Mgusu iliyoko katika Halmashauri ya Mji wa Geita ambapo mafanikio hayo yameonekana katika kipindi cha uongozi wa awamu ya tano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yamewawezesha wananchi wa Kata ya Mgusu na mitaa yake kujivunia mema ya nchi yao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii hivi karibuni alipotembelewa katika kata yake, Diwani wa Kata ya Mgusu Mheshimiwa Pastory Ruhusa ameishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watendaji walio chini yake hususan wa Mkoa na Wilaya ya Geita kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuhakikisha Kata ya Mgusu inapata huduma za muhimu za kijamii.
Mhe. Ruhusa amesema kuwa kwa sasa Kata yake imefanikiwa kujenga shule mbili za Sekondari ambazo ni Shule ya Sekondari Mgusu na Shule ya Sekondari Nyakabale ambazo shule zote zilifunguliwa mapema mwaka 2019, Shule ya msingi Manga iliyoko katika mtaa wa Manga, Pia ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Machinjioni, ujenzi wa Zahanati ya Mgusu, Ujenzi wa Maabara ya masomo ya sayansi, madarasa mawili na jengo la utawala Shule ya Sekondari Mgusu bado unaendelea.
“Haikuwa jambo rahisi kujenga shule mbili za Sekondari kwa wakati mmoja katika kata yangu, lakini napenda kuwapongeza na kuwashukuru kwa dhati wananchi wangu kwa kujitoa kwa moyo kushirikiana na Halmashauri ya mji wa Geita katika shughuli za ujenzi wa shule hizi baada ya kutambua namna wanafunzi hususani wa kike wanavyopata shida kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita kumi kwenda shule ya Sekondari Shantamine iliyoko katika kata ya jirani ya Mtakuja.” Aliongeza Mhe. Ruhusa
Akiongea kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Mgusu Bi. Ziara Peter ambaye ni mkazi wa mtaa wa Mgusu ametoa shukrani za dhati kwa Diwani wa kata yao na Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kuwawezesha wananchi wa kata hiyo kupata umeme wa uhakika tofauti na awali walipokuwa wanaishi gizani. Pia wameishukuru Serikali kwa kuwajengea zahanati ambayo baadaya kukamilika itaondoa adha ya kina mama wajawazito kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya kujifungua.
Kata ya Mgusu ni mojawapo ya kata changa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita, ambapo sehemu kubwa ya wakazi wake hujishughulisha na uchimbaji mdogo wa madini ya Dhahabu, ilianzishwa rasmi mwaka 2015 ikiwa na mitaa minne ambayo ni Nyakabale, Manga, Machinjioni na Mgusu. Uongozi wa kata ulipoanza kazi walikuwa na shule mbili za msingi na Zahanati ya Nyakabale pekee, wananchi wa kata hiyo hawakuwa na huduma ya nishati ya umeme wala maji.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa