Mgogoro wa Vigingi na Mipasuko kumalizwa Geita
Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde amewaahidi wananchi wa Halmashauri ya Mji Geita kuwa migogoro ya vigingi na mipasuko iliyodumu kwa miaka mingi itamalizwa kwa amani bila migongano ya namna yoyote.
Mhe. Mavunde ametoa kauli hiyo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na wananchi wa mitaa ya Nyakabale, Manga, Nyamalembo, Samina na Katoma wakati wa mikutano ya hadhara iliyofanyika katika maeneo yao.
Waziri wa Madini ameeleza kuwa Serikali kupitia wizara yake imeweka mkakati wa kuhakikisha mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 baina ya wananchi hao na Mgodi wa Dhahabu Geita ndio maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuelekeza kutembelea maeneo hayo na kuzungumza na wananchi ili kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
“Naomba nitumie nafasi hii kupongeza jitihada zilizofanywa na mtangulizi wangu upande wa Wizara ya Madini Mhe. Dkt. Doto Biteko ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kazi nzuri ambayo aliianza katika kutatua changamoto hii ambapo kupitia kazi yake kumenirahisishia kazi yangu kuwa nyepesi katika kuelekea kupatikana kwa ufumbuzi wa mgogoro huu.” Aliongeza Mhe.Mavunde.
Mbunge wa Jimbo la Geita mjini Mheshimiwa Costantine Kanyasu amesema kuwa tatizo la vigingi limedumu kwa miaka mingi na amekuwa mstari wa mbele kuliwasilisha serikalini hususan anapokuwa katika vikao vya bunge, hivyo ameishukuru Serikali kwa namna inavyoendelea kusikiliza kilio cha wananchi hao na kupongeza hatua iliyofikiwa kwa sasa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela aliwapongeza wananchi wanaoishi katika mitaa inayozunguka mgodi wa GGM kwa kuendelea kuwa wavumilivu wakati wote ambapo Serikali inafuatilia mgogoro huo na kuwasihi kuendelea kuiamini Serikali kwani miezi michache mbeleni inakwenda kutatua mgogoro huo kwa weledi mkubwa.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa