Halmashauri Zatakiwa Kutumia Vyema Mfumo wa Mapato
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Angelina L. Mabula ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Geita kuhakikisha mafaili yote ya ardhi na viwanja yanaingizwa katika mfumo wa usimamizi na ukusanyaji kodi za ardhi na Majengo kielektroniki kufikia Septemba 30 mwaka 2017.
Mh. Angelina Mabula ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha hitimisho la ziara yake katika Mkoa wa Geita kilichofanyika tarehe 29/8/2017 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pia amewaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa wa Geita kuwawajibisha Wakuu wa Idara za Ardhi na Maafisa Ardhi wateule ambao watashindwa kutekeleza agizo hilo katika muda husika. Pia ameagiza kuwa viwanja vyote ambavyo havina upimaji wa kudumu (demarcation) vikamilishwe ili kuziwezesha Halmashauri kupata mapato.
Mh. Angelina Mabula ametoa agizo kwa Mkoa wa Geita kufanya upimaji shirikishi katika miji inayokuwa kwa kasi ili kuifanya iwe katika mpangilio na kuwezesha watu kukaa katika utaratibu uliokusudiwa. Pia kila robo ya mwaka wa fedha idadi ya wadaiwa sugu ianishwe na wadaiwa hao wapewe hati ya madai( demand note) ili walipe madeni hayo na kuongeza mapato ya Halmashauri na Serikali kwa ujumla.
“Maafisa Ardhi pangeni utaratibu mzuri wa utendaji kazi na Asilimia 30% ya mapato inayorudishwa na Wizara ya Ardhi katika Halmashauri inatakiwa itumike katika kuwawezesha wataalamu wa Idara ya Ardhi kununua vitendea kazi na kuboresha mazingira ya Ofisi zao. Nawasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote kutotumia fedha hizo katika shughuli nyingine tofauti na Idara ya Ardhi”. Aliongeza Mh.Angelina Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi amewataka Maafisa Ardhi kutatua kwa wakati malalamiko yanaowasilishwa kwenye ofisi zao na kuzitaka Halmashauri kuwashirikisha Makatibu Tawala wa Mkoa na Makamishna wa Ardhi wa Kanda katika utatuzi wa migogoro mbalimbali ya Ardhi na kupanga mikakati ya upimaji katika maeneo yao. Kadhalika ameagiza kutochukua maeneo ya watu pasipo kuwepo fedha ya fidia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita Mh. Leonard K. Bugomola amesema Halmashauri yake imepokea maagizo yote yaliyotolewa na Niabu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kuahidi kuyafanyia kazi kikamilifu kwa maendeleo ya Mkoa wa Geita na Taifa kwa ujumla.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa