Mbolea Kuanza Kusambazwa na Vyama Vya Ushirika
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika msimu wa kilimo 2023/2024. imejipanga kutumia vyama vya ushirika kufikisha mbolea kwa wakulima ambapo kampuni ya mbolea Tanzania itawezesha kufikisha mbolea kwenye maeneo yasiyofikika na hivyo kuwapunguzia kero ya umbali wakulima kutokwenda Zaidi ya kilomita 15 kufuata pembejeo ya mbolea.
Mipango hiyo imebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku Ndg. Louis Kasera alipokuwa akizungumza katika kikao cha kuwajengea uwezo wataalam wa Idara ya Kilimo na mifugo, Mrajis na viongozi wa vyama vya ushirika mkoani Geita juu ya namna bora ya kufikisha mbolea kwa wakulima kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Ndg. Kasera ameeleza kuwa ifikapo tarehe mosi ya mwezi Julai mbolea zitakuwa zimesogezwa karibu na wakulima na kutoa wito kwa wakulima kujitokeza kununua mbolea mapema ili kupunguza misururu mirefu wakati wa msimu na kusema kwamba nguvu kubwa itawekwa kwenye vyama vya ushirika ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wakulima.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Profesa Godius Kahyarara amepongeza uamuzi wa Serikali wa kutumia vyama vya ushirika katika kusambaza mbole kwa msimu wa kilimo 2023/2024 na kuongeza kuwa vyama vya ushirika vinaishi na wananchi katika maeneo yao hivyo vinatambua changamoto zote zinazowakabili wakulima katika upatikanaji wa pembejeo za kilimo.
Profesa Kahyarara ameiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya mbolea vya ndani ili kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi na kuongezaa kuwa uzalishaji wa ndani utaongeza ufanisi Zaidi katika kukuza kilimo na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza mbolea nje ya nchi na baadaye kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku, Louis Kasera alieleza lengo la kufika mkoani hapo ni Pamoja na kuhamasisha watendaji kuendelea na zoezi la usajili na uhuishaji wa taarifa za wakulima ili kuwawezesha kunufaika na mbolea za ruzuku kwa msimu wa kilimo 2023/2024.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa