Wananchi Wahimizwa Kuwekeza Katika Elimu
Wakazi katika Halmashauri ya Mji Geita wamehimizwa kuhakikisha kuwa wanatumia nguvu zao na raslimali walizonazo kuwekeza katika sekta ya Elimu ili kupambana na adui ujinga na kujenga Taifa litakalozalisha wataalamu katika fani mbalimbali ambao watailetea nchi ya Tanzania maendeleo makubwa.
Rai hiyo imetolewa na Mkimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2018 Ndugu, Charles Francis Kabeho alipokuwa akizindua rasmi madarasa mawili, bwalo la chakula na bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kasamwa wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Mji Geita tarehe 01/04/2018.
Mkimbiza Mwenge wa Uhuru 2018 amewasihi wananchi kuwekeza katika elimu kwa kushiriki kuchangia ujenzi wa madarasa, mabweni, utengenezaji wa madawati na kujenga vyuo vya ufundi na ufundi stadi ili kuwapa nafasi wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kukosa nafasi ya kuendelea na kidato cha tano wapate fursa ya kupata elimu ya ufundi.
Ndg. Kabeho aliwapongeza wananchi wa Kata ya Kasamwa na vitongoji vyake kwa kujitoa kikamilifu katika kuchangia fedha na nguvu kazi wakati wa zoezi la ujenzi wa miundombinu hiyo. Aliongeza kuwa wananchi hao wameonyesha namna walivyotambua umuhimu wa elimu katika eneo lao.
Mkibiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018 amewaasa wazazi na walezi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao katika kuwanunulia watoto wao mahitaji muhimu yanayohitajika shule kama sare za shule, madaftari ili kutoruhusu nafasi ya watoto wao kushindwa kuhudhuria masomo kwa kukosa mahitaji ya msingi.
“Wazazi jitahidini kuwahimiza watoto na vijana wenu kupenda masomo ya sayansi na hisabati ili kupata watu watakaotumika katika uzalishaji wa viwanda mbalimbali vinavyoanzishwa nchini na kupata wataalam wa masomo ya sayansi.” Aliongeza Ndg. Charles Kabeho.
Ndg. Charles Kabeho alitumia fursa hiyo kuwaagiza wazazi na walezi wote kufuatilia mahudhurio ya wanafunzi shuleni ili kupunguza tatizo la utoro shuleni. Pia aliziagiza idara za Elimu Msingi na Sekondari kufuatilia na kuchukua hatua madhubuti katika kuondokana na tatizo la utoro shuleni, ambapo Mkoa wa Geita ni wa pili kwa tatizo la utoro shuleni kwa asilimia 8.1
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Kasamwa Bi. Agness D. Busanji amepokea agizo hilo na kuahidi kufuatilia kikamilifu mahudhurio ya wanafunzi katika shule yake na kubaini changamoto mablimbali zinazopelekea wanafunzi hao hususani wa kike kutoroka shule, ili wazitatue kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji.
Miundombinu ya madarasa, bwalo la chakula na bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Kasamwa limegharimu kiasi cha Shilingi 444,680,300.00 chanzo cha fedha hizo ni mapato ya ndani ya Halmashauri na mchango wa wananchi. Mradi huo ni moja ya mradi kati ya miradi tisa iliyowekewa mawe ya msingi, kuzinduliwa, kufunguliwa na kutembelewa na Mwenge wa Uhuru 2018 katikaHalmashauri ya Mji Geita, ambapo kwa ujumla wake imegharimu Shilingi 3,374,178,963.00.
Kauli Mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2018 ni “Elimu ni Ufunguo wa Maisha Wekeza sasa kwa Maendeleo ya Taifa letu”.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa