Mashindano ya Olimpiki maalum yaanza kwa kishindo Geita Mji
Mashindano yanayowashirikisha wanafunzi na watu wenye ulemavu wa akili yanayofahamika kama Olimpiki maalum( special Olympics) yamefunguliwa rasmi katika Halmashauri ya Mji Geita ambapo wanafunzi wenye ulemavu kutoka katika shule tano zinazofundisha elimu maalum wanashiriki mashindano hayo.
Akifungua rasmi mashindano hayo, Afisa Michezo wa Halmashauri ya Mji Geita Bi. Juliana Kimaro amewaagiza waratibu wa mashindano hayo kuchagua wanafunzi watakaomudu vyema michezo inayoshindaniwa na wajitahidi kuonyesha nidhamu katika mashindano hayo.
Mratibu wa mashindano hayo Mwl. Thomas Sabuka kutoka Shule ya Msingi Kasamwa ameeleza malengo ya mashindano hayo kuwa ni kuwapa fursa watu wote wenye ulemavu wa akili kupata fursa ya kuwa raia wenye manufaa, pia kuwa wazalishaji wanaokubalika na kuheshimika katika jamii zao.
Timu ya wanafunzi kutoka Halmashauri ya Mji Geita itaungana na timu kutoka Halmashauri za mkoa wa Geita ambazo zitaunda timu ya Mkoa wa Geita itakayoshiriki mashindano hayo yatakayoanza Tarehe 6-13/12/2017 mjini Zanzibar.
Mashindano ya Olimpiki maalum yalianzishwa na Bi. Eunice Kenedy Shriver mwaka 1968 huko Marekani na kushirikisha wanamichezo 1000 ambao walitoka katika mabara matano ulimwenguni. Tanzania ilianza kushiriki mashindano hayo kidunia mwaka 1986 ikiwa ni miongoni mwa nchi 200 zinazoshiriki mashindano hayo kwa sasa.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa