Mapato Ya Ndani Kujenga Miradi Ya Kimkakati
Halmashauri ya Mji wa Geita katika kipindi cha pili ndani ya Serikali ya awamu ya tano imejipanga kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa kutumia chanzo cha mapato ya ndani ya Halmashauri tofauti na hali iliyokuwepo awali.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mheshimiwa Costantine Morandi wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani robo ya pili kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Ofisi kuu Halmashauri ya Mji Geita.
Mhe. Morandi amesema kuwa miradi mikubwa kama ujenzi wa masoko na machinjio ya kisasa imetekelezwa kupitia fedha zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita kwa jamii inayowazunguka( CSR) lakini Halmashauri ya Mji inaongoza katika ukusanyaji wa mapato kuliko Halmashauri zote za Miji Tanzania Bara, hivyo inatakiwa fedha hizo zifanye mambo makubwa na ya mfano.
“Halmashauri ya Mji Geita tumepanga kutoka kwenye dhana ya CSR na kufanya thamani ya makusanyo yetu ya ndani kuonekana, tunatakiwa tujenge Zahanati nzuri na za kisasa, Shule za msingi na Sekondari, masoko ya kisasa pamoja na miradi mingine kuanzia msingi mpaka ukamilishaji kwa kutumia fedha za mapato ya ndani tukisaidiwa na nguvu za wananchi na si kutegemea fedha za CSR katika kutekeleza miradi hiyo”. Aliongeza Mhe. Morandi.
Akisoma changamoto mbalimbali zilizopo katika kata zote za Halmashauri ya Mji wa Geita, Diwani wa Kata ya Nyanguku Mheshimiwa Elias Ngole amesema kuwa upungufu wa vyumba vya madarasa kwa shule zote na ubovu wa mabarabara ambazo zimeharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha ni miiongoni mwa vikwazo vinavyowakabili wananchi walioko kwenye maeneo yao ya utawala.
Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Mji Geita Bi. Magreth Macha amesema kuwa Halmashauri ya Mji Geita itaendelea kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa kwa kujenga vyumba zaidi kulingana na upatikanaji wa fedha. Kadhalika Mamlaka ya Elimu Tanzania imeridhia kujenga Mabara moja ya masomo ya sayansi katika Shule ya Sekondari Nyanza.
Katika hatua nyingine Halmashauri ya Mji wa Geita imetenge shilingi 150,000,000/= katika bajeti yake ya mwaka 2021/2022 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Shiloleli na shilingi 50,000,000/= kwa lengo la kununua maeneo ya kujenga shule mpya ya sekondari ndani ya Kata ya Buhalahala,
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa