Maonyesho ya Expo Dubai Yaleta Neema Geita
Miezi michache baada ya kupita kwa maonyesho ya kidunia ya Expo Dubai ujumbe wa wawekezaji kutoka Umoja wa falme za kiarabu-Dubai wamefika mkoani Geita hususan Halmashauri ya Mji Geita kwa nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Wawekezaji hao wakiongozwa na wakili Walid Jumaa wamesema kuwa baada ya kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Geita kwenye maonyesho ya Expo Dubai walipata fursa ya kubadilishana mawazo na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Rosemary Senyamule ambaye aliwakaribisha kuja kujionea fursa mbalimbali zilizopo mkoani kwake.
Wakili Walid Jumaa ameeleza kuwa wamefika Geita kwa lengo la kupafahamu na kujionea maeneo kadhaa ya uwekezaji katika sekta mbalimbali ambapo wakati wa ziara yao Tarehe 14/6/2022 walipata fursa ya kutembelea na kujifunza namna machinjio ya kisasa Mpomvu itakavyofanya kazi mara baada ya ujenzi kukamilika hivi karibuni, namna Soko kuu la Dhahabu Geita mjini linavyochangia katika ukuzaji wa pato la mkoa na Taifa na kutembelea maeneo ya viwanja vilivyotengwa mahsusi kwa shughuli za uwekezaji na viwanda.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amesema kuwa wawekezaji hao wameonesha nia ya kuwekeza katika kujenga kituo cha kimataifa cha usuluhishi wa migogoro ya kibiashara,kuwekeza katika sekta ya uchimbaji madini, sekta ya utalii, sekta ya elimu na afya , kukuza sekta ya kilimo na mifugo pamoja na ujenzi wa viwanda vya madawa na chakula katika mkoa wa Geita.
“Baada ya majadiliano na wageni wetu, wameonesha sahuku ya kuifanya Geita kuwa Dubai ya Afrika na kwa dhamira hiyo tarehe ya leo tunasaini kwa pamoja mkataba wa awali wa makubaliano baina yao na Serikali juu ya namna tutakavyoendelea kuibadilisha Geita katika sekta mbalimbali.” Aliongeza Mhe. Rosemary Senyamule.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uhamasishaji uwekezaji EPZA Ndg. James Maziku amesema kuwa uwepo wa wawekezaji ndani ya mkoa wa Geita kutaongeza ukuaji wa uchumi ndani ya mkoa pamoja na kuzalisha ajira kwa wingi kwa wakazi wa mkoa huo. Kadhalika ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuitambulisha nchi kimataifa na kufungua milango kwa wakezaji kuja kuwekeza Tanzania.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa